Chato kuunganishwa mkongo wa taifa

SERIKALI kupitia Wizara ya Habari na Mawasiliano imetenga Sh bilioni 1.8 kwa ajili ya kuiunganisha wilaya ya Chato kwenye huduma ya mkongo wa taifa ili kuimarisha mfumo wa mawasiliano, ulinzi na usalama.

Naibu Waziri wa Habari na Mawasiliano, Mhandisi Kundo Mathew amebainisha hayo wilayani Chato alipofika kukagua maendeleo ya mradi huo eneo la Kitela mjini Chato.

Kundo amesema wizara yake imejidhatiti kusimamia kikamilifu ujenzi wa mradi huo ukamilike kwa wakati na kufanikisha adhima ya serikali kuifanya Chato iwe na huduma bora.

Advertisement

“Niwahakikishie kwamba sasa Chato inaenda kuwa salama kwa upande wa mawasiliano, kwa sababu mawasiliano ni uchumi, mawasilinao ni haki kulingana na ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).” amesema Kundo.

Amesema, katika kuimarisha usimamizi wa miradi ya mawasiliano serikali imetumia Sh bilioni 7.28 kununua magari 45 kwa ajili ya kuhakiki na kusimamia ujenzi wa mkongo wa taifa ikiwemo minara 758 inayojengwa nchi nzima iweze kukamilika kwa wakati.

Amewahakikishia watanzania ifikapo Mei 2025 minara hiyo itakuwa imekamilika na punde itazindua ujenzi wa minara mingine 636 ikiwemo minara 21 maalum ya kuboresha huduma za utangazaji.

“Natoa maelekezo nchi nzima katika ujenzi wa Kilomita 4,442 za mkongo wa taifa na ujenzi wa vituo vyote naomba nielekeze ujenzi uende kwa kasi na ukamilike kwa wakati.”Amesema

Nae, Meneja wa Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL) Mkoa wa Kagera wanaohudumia Chato, Theopister Mark amefafanua Sh bilioni 1.8 inajumuisha gharama za ujenzi wa mkongo wa Km 56 kutoka eneo la Bwanga mpaka Chato uliogharimu Sh milioni 776.76.

Amesema gharama ya vifaa vya mawasiliano ambavyo vitafungwa katika jengo la TTCL Chato ni Sh milioni 517.83 huku mitambo ya umeme ambayo itafungwa hapo itagharimu Sh milioni 284.68.

“Kituo hiki baada ya kukamilika kitakuwa na uwezo wa kasi ya 4GB kwa sekunde. Urefu wa kuunganisha mtambo ni Kilomita 120 kutokea kituo cha Geita TTCL kuja kituo cha TTCL Chato,”amesema.

Amesisitiza mkongo wa taifa Chato utaongeza kasi ya mtandao na kuboresha huduma mtandao ikiwemo serikali mtandao, afya mtandao, mikutano ya mtandao pamoja na elimu mtandao.

Pia, amesema utakuza mapato serikalini ambapo kiasi cha dola za kimarekani milioni 101 zimezalishwa kati ya mwaka 2010 – 2022 na kuimarisha usalama wa wilaya, mkoa na taifa.

Mkuu wa Wilaya ya Chato, Deusdedith Katwale amekiri mkongo wa taifa unaenda kuchagiza huduma za kidijitali na kukuza maendeleo ya sekta ya utalii wilayani humo kupitia hifadhi za taifa za Rubondo na Burigi.