CHELSEA itakuwa na kazi ngumu ya kuhakikisha inapindua matokeo ya mchezo uliopita wakati timu hiyo itakaporudiana na Dortmund katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa utakaopigwa leo Stanford Bridge.
Mchezo wa raundi ya kwanza, Chelsea ilipoteza bao 1-0 bao la Karim Adeyemi. Ushindi wao dhidi ya Leeds wikiendi iliyopita huenda ukafufua matumaini ya Chelsea kuelekea mchezo wa leo.
Kuelekea mchezo huo, Reece James, Christian Pulisic huenda wakarejea uwanjani, huku beki Thiago Silva atakosekana kutokana na majeraha. Mason Mount atakosekana baada ya kupokea kadi ya njano.
Dortmund, inayoshika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao nyuma ya Bayern Munich kwenye Bundesliga, inasafiri hadi London ikitaka kuandika ushindi wa 11 mfululizo katika michuano yote, huku Chelsea ikitumai kupata ushindi mfululizo kwa mara ya kwanza tangu Oktoba.
Ili kusonga mbele, vijana wa Graham Potter watalazimika kufunga mabao mawili kwenye mechi kwa mara ya kwanza tangu tarehe 27 Disemba.
Chelsea pia wanaingia kwenye kinyang’anyiro hicho wakiwa wametupwa nje ya vikombe viwili vya nyumbani na wako nafasi ya 10 kwenye Ligi ya Kuu, ambayo inaacha Ligi ya Mabingwa ikiwa ni fursa yao pekee ya kushinda kombe.
Mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa utakuwa kati ya Benfica dhidi ya Club Brugge, michezo yote itapigwa saa 5: 00 usiku.