China kuitumia Tanzania kuzalisha bidhaa za ngozi

KAMPUNI ya kuzalisha bidhaa za ngozi vikiwemo viatu ya Huajian Group ya China inajipanga kuja kuwekeza nchini kuanzia mwaka huu.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema hayo alipozungumza na HabariLEO.

Kairuki alisema alikutana na  mmiliki wa Kampuni hiyo, Huarong Zhang, hivi karibuni nchini humo na ameahidi kuja kuwekeza hapa nchini.

Alisema kampuni ya Huajian Group  inamiliki viwanda vya kuzalisha bidhaa za ngozi nchini China na sehemu mbalimbali duniani ikiwemo nchini Ethiopia.

“Kampuni hii imewekeza sana nchini Ethiopia, sasa wanapanga kuwekeza Tanzania pia. Mmiliki wake alikutana na mimi mwezi Machi na kuelezea nia yake ya kutaka kuwekeza Tanzania,” alisema Kairuki.

Pia alisema mmiliki wa Kampuni hiyo alikutana na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, alipofanya ziara nchini  China mwezi uliopita.

Alisema mwezi huo huo Aprili Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Uwekezaji, Dk Tausi Kida, alitembelea eneo la uwekezaji la kampuni hiyo nchini Ethiopia ili  kuona uwekezaji mkubwa uliofanyika.

“Sasa huyu bwana atakuja Tanzania mwezi Mei kati kati ya wiki ya pili kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu fursa za kujenga kongani ya viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za ngozi na bidhaa nyingine ambazo malighafi zake zinapatikana hapa nchini kwa urahisi'”alisema Balozi Kairuki.

Kwa mujibu wa Kairuki, uamuzi wa kampuni hiyo kutaka kuwekeza nchini kwa kujenga viwanda vya bidhaa ngozi ni maendeleo makubwa yatakayokuwa na matokeo chanya kwa uchumi nchi hii.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button