China, Tanzania kuimarisha ulinzi

SERIKALI ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China zitaendelea kushirikiana kupambana na vitisho vyote vya usalama katika kuimalisha ulinzi wa nchi hizo mbili. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Innocent Bashungwa ameeleza.

Akizungumza Julai 12, 2023 katika Maadhimisho ya Miaka 96 ya Jeshi la Ukombozi la China, Waziri Bashungwa ameeleza kuna baadhi ya changamoto za usalama ambazo ili kuzimaliza juhudi za pamoja zinahitajika.

Advertisement

“Kutokana na hali hii kwamba, tutaendelea kumtazama rafiki yetu China na marafiki wengine duniani kote, katika kushughulikia changamoto hizi za usalama kwa ajili ya amani na usalama endelevu duniani.”Amesema Bashungwa.


Akisoma hotuba yake katika Ubalozi wa China, Bashungwa alisema uhusiano baina ya nchi hizo mbili ni mkubwa ulioanza tangu enzi za Mwenyekiti, Mao Zedong na Hayati Julius Nyerere, suala lililopelekea msingi imara ambao PLA na JWTZ, wamefanya usaidizi usioyumba, ushirika, na ushirikiano katika maeneo kadhaa ya mafunzo ya kijeshi.

Balozi wa China, Tanzania Chen Mingjian amesema mwaka 2024 China na Tanzania zitaazimisha miaka 60 ya uhusiano wa kidiplomasia ikiwa ni historia ndefu ya mabadilishano ya kirafiki.

Amesema China imekuwa rafiki mkubwa wa Tanzania katika kuweka maendeleo ya uhusiano wa kirafiki katika nafasi muhimu na siku zote nchi hizo zimekuwa ndugu, marafiki waaminifu na washirika wa dhati.

“Katika miaka ya hivi karibuni, kwa mwongozo wa wakuu wa nchi hizo mbili, uhusiano kati ya China na Tanzania umeendelea kwa kasi na kwa njia ya pande zote. China imesalia kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Tanzania na chanzo kikubwa cha uwekezaji wa kigeni kwa miaka mingi.” Alisema Balozi Mingjian.

Balozi huyo alisema Jengo la Ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania jijini Dar es Salaam, jengo jipya la Chuo cha Taifa cha Ulinzi na Kituo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi Kagera, vilijengwa kwa msaada wa China, vyote vimekamilika na kuanza kutumika, hatua hiyo inaonesha uhusiano mzuri wa mataifa hayo.

“Miradi mikubwa iliyofanywa na makampuni ya China, kama vile ujenzi wa sehemu ya tano na sita ya Reli ya Standard Gauge, Kituo cha Umeme wa Maji cha Julius Nyerere, upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam umeendelea kwa kasi.” Alisema Mingjian.

Amesema siku za usoni China daima itatazama uhusiano baina ya Tanzania kwa mtazamo wa kimkakati na kuwa mrafiki mwaminifu wa Tanzania.

“Tutaendeleza kasi ya ubadilishanaji na mazungumzo ya hali ya juu, kupanua kiwango cha biashara baina ya nchi, kuimarisha mawasiliano kati ya watu na watu na utamaduni, kuimarisha ushirikiano katika mazingira ya kimataifa.”

Alisema ana imani kubwa kuwa urafiki kati ya China na Tanzania utaendelea kustawi na kuchanua katika siku zijazo.

2 comments

Comments are closed.