China tayari kuboresha miundombinu ya Tazara
SERIKALI ya China imesema ipo tayari kuboresha miundombinu ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) iwe na tija zaidi.
Naibu Balozi wa China nchini Tanzania, Suo Peng amesema hayo Dar es Salaam jana wakati wa kumbukumbu ya wafanyakazi na mafundi wa Kichina 65 waliopoteza maisha wakati wa ujenzi wa reli ya Tazara.
Kumbukumbu hiyo ilifanywa kwa kuweka mashada ya maua katika mnara na makaburi hayo katika eneo la Gongolamboto.
“China, Tanzania na Zambia zimefikia makubaliano ya kufufua reli ya Tazara ili kuleta uhai mpya wa reli yenye manufaa ya ustawi na maendeleo endelevu,” alisema Peng.
Alisema ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa kilometa 1,860 kwa miaka sita uliunganisha Tanzania na Zambia na imeendelea kutoa huduma za usafiri wa mizigo na abiria.
Peng alisema hivi sasa ushirikiano wa kikanda barani Afrika umeshamiri hivyo ni muhimu mataifa hayo yawe na mtandao wa uunganishaji wa miundombinu ili kurahisisha huduma na biashara.
Alisema uhusiano wa China na Tanzania umeendelea kuimarika katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mikopo nafuu ya kujenga miradi ya kimkakati yenye maslahi ya kukuza ustawi wa jamii.
Peng alisema miundombinu ya reli ni muhimu kwa maendeleo endelevu kwa sababu hutumika kubeba mizigo, abiria na kuleta chachu ya ukuaji wa uchumi na kusisitiza kuwa ukitaka kuwa tajiri jenga reli.
Alisema biashara baina ya China na Tanzania kwa mwaka 2022 iliongezeka kwa asilimia 23.7.
Awali Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete alisema Tanzania inathamini mchango uliotolewa na China katika kujenga reli ambayo imekuwa na tija kwa taifa.
Aidha, alisema reli hiyo kwa sasa haina ufanisi kama ilivyokuwa awali kutokana na uchakavu wa miundombinu.
“Tanzania inathamini mchango mkubwa uliotolewa na China katika ujenzi wa reli ya Tazara na katika miradi mingine nchini, tutaendelea kuthamini na kuwaenzi wale wote waliokufa wakati wa kujenga miundombinu hii,” alisema Mwakibete.
Ofisa Mtendaji wa Tazara-Tanzania, Bruno Ching’andu alisema ujenzi wa reli hiyo umekuwa na manufaa kwa sababu umewezesha kusafirisha mizigo kati ya Tanzania na Zambia na hiyo imeleta tija ya uchumi.
Hata hivyo, alisema ili kuleta tija zaidi, maboresho ya miundombinu na vifaa katika reli hiyo yanahitajika ili kuongeza usafirishaji wa mizigo kati ya Bandari ya Dar es Salaam na Zambia.