UBALOZI wa Tanzania nchini China umesema filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’ imeoneshwa katika mtandao maarufu wa Haokan nchini China.
Kupitia ukurasa mtandao wa kijamii wa twitter, ubalozi huo umeeleza kuwa zaidi ya watu milioni moja walikuwa wameitazama kupitia Haokan ndani ya siku tatu.
Pia Ubalozi Mdogo wa Tanzania Guangzhou umeeleza kuwa Kampuni ya Guangzhou Intergrated Marketing Company (GIMC) yenye mtandao nchini humo ikiwa na wateja wa kampuni za ndani na nje zaidi ya 300, imekubali kusaidia kutangaza bidhaa na utalii wa Tanzania katika soko la China.
Katika ukurasa wake wa twitter, ubalozi huo ulieleza kuwa pia GIMC imekubali ofisi ya Konseli Kuu kutumia ukumbi wake wa filamu kuzindua filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’ kwa mawakala wa tiketi za ndege na kampuni za waongoza watalii jijini Guangzhou.
“Tanzania pia imepewa fursa ya kuweka majarida na vipeperushi vya utalii katika maktaba yao na bidhaa za Tanzania katika mgahawa wao. Sehemu hizo za huduma hutumiwa na wafanyakazi na wanafunzi wengi kwa kuwa zipo katika viwanja maarufu vya maonesho ya biashara vya Canton,” ulieleza ubalozi huo.
Wiki kadhaa zilizopita Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa filamu hiyo imerahisisha kazi ya kutangaza vivutio vya utalii nchini na uzuri wa Tanzania kwa ujumla.
Balozi Kairuki alisema kwa mara ya kwanza Julai 30, mwaka huu filamu hiyo ilioneshwa kwenye Kituo cha Televisheni cha Hainan nchini humo na kutazamwa na watu milioni 7.5.
Alisema wametafsiri filamu hiyo kwa lugha ya Kichina na ilioneshwa pia kwenye mtandao wa Bilibili wenye wafuatiliaji 750,000.
“Lengo letu sasa ni kuona Wachina wengi wanafahamu vivutio vya Tanzania na kufanya uamuzi wa kutalii Tanzania ili waache madola ya kutosha kwa Watanzania wenzetu wanaofanya shughuli za utalii,” alisema Balozi Kairuki.
Alisema watalii kutoka China wana sifa ya kutumia fedha nyingi wanapokwenda kutalii hivyo wakija Tanzania kuanzia sherehe ya mwaka mpya wa Kichina, Watanzania waliopo kwenye sekta ya utalii watanufaika.
“Na hii ndio habari Mama Samia anataka kwa ajili ya Watanzania, wapate kipato waondokane na umaskini na wawe matajiri, kuwa tajiri sio dhambi, tunataka Watanzania wafaidike na hela ya utalii,” alisema.
Hivi karibuni, Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi katika Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Daniel Masolwa alisema filamu ya ‘Tanzania: The Royal Tour’ imehamasisha na kuongeza watalii kuingia nchini kutoka 456,266 hadi kufikia 742,133 sawa na ongezeko la asilimia 62.7.
Comments are closed.