Chissano asisitiziza matumizi ya Kiswahili

RAIS Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chisano amezitaka nchi za Afrika Mashariki kuendeleza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika maeneo muhimu ya kiutawala na kijamii.

Chisano, ameyasema hayo katika hafla ya utoaji Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambapo amesema Kiswahili ni tunu na utambulisho wa Afrika na Mwafrika

Amesema, Kiswahili ni lugha yetu ya Afrika hivyo hakuna budi kuilinda na kuikuza kwa kuipa heshima na dhima mbalimbali mathalani kutumika katika elimu, siasa, utawala na masuala mengine ya kijamii.

“Ninatoa wito kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Mabaraza ya Kiswahili ya nchi wanachama kuendeleza matumizi ya Kiswahili katika maeneo muhimu ya kiutawala na kijamii kwani Kiswahili ni tunu na utambulisho wa Afrika na Mwafrika.”Amesisitiza

Aidha Chisano, ameipongeza Tanzania kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuona umuhimu wa kuenzi, kuiendeleza, na kuikuza lugha adhimu ya Kiswahili kupitia shindano la uandishi bunifu.

“Kama tujuavyo, lugha ya Kiswahili ina historia kubwa katika ukombozi wa bara la Afrika. Vilevile, lugha ya Kiswahili ni lugha rasmi katika Umoja wa Afrika na inazungumzwa takribani katika mabara yote.

“ Hivyo, utoaji wa Tuzo za Ubunifu ni kuendelea kutambua thamani muhimu kabisa ya lugha ya Kiswahili hapa nchini na Afrika kwa ujumla. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.”Amesema

Rais Chisano pia, amewapongeza Watanzania, kwa kutambua na kuenzi mchango wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere katika kukuza lugha ya Kiswahili.

“Ni wazi kabisa Mwalimu Nyerere kwa dhati kabisa, aliikuza lugha ya Kiswahili kwa kuandika maandiko bunifu kama mashairi, riwaya na kutafsiri kazi mbalimbali za fasihi ya Kiingereza katika Kiswahili. Hivyo, ni heshima kubwa tuzo hii kupewa jina la Mwalimu Nyerere.

“Pia, ni fahari kubwa kwangu kupata heshima ya kuwa mgeni rasmi katika halfa ya tuzo hii ya mwaka 2023.”Amesema

Amesema, Kiswahili nyumbani kwake ni Tanzania; hivyo, juhudi kama hizi za kutambua mchango wa wadau wa maandiko bunifu kwa lugha ya Kiswahili ni kitu muhimu sana.
“Ni maoni yangu kuwa juhudi hizi ziendelezwe bila ukomo kwani uhai wa lugha yoyote iwayo duniani, ni kuwapo na machapisho yaliyoandikwa kwa lugha hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button