Chongolo aiagiza Takukuru kuchunguza bili za maji Morogoro

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wa bili na bei za maji kwa wananchi wilayani Malinyi mkoani Morogoro ili kupata ukweli iwapo wananchi hao wanabambikiwa bili au lah.

Kauli hiyo ameitoa leo katika Kata ya Mtimbila aliposimamishwa na wananchi akiwa katika msafara wake kuelekea Makao Makuu ya Wilaya ya Malinyi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya CCM.

Mara baada ya kusimamishwa eneo hilo na wananchi walitoa kero yao kuwa bili ya maji ni sambamba na gharama za kununua maji ambapo pamoja na kwamba chanzo cha maji ni cha mserereko lakini bado wanatozwa shilingi 100 kwa ndoo ya lita 20.

Advertisement

Aidha,wamema bei ya maji wanayotozwa kwa mwezi kwa wale ambao hawajafungiwa mita za maji za ni shilingi 7,000 na bili hiyo inalipwa kila mwezi hata kama maji hayatoki.

Akijibu kero hiyo ambayo pia imetolewa na wananchi katika Wilaya ya Kilombero,Chongolo aliagiza Takukuru kufanya uchunguzi ili kuona uhalali wa bei hizo kwani mwongozo wa malipo ya maji ya chanzo hicho ni shilingi 20, kwa ndoo moja ya maji ya lita 20.

“Takukuru,hili lichukueni lichunguzeni kuona uhalali wake,maana nimepewa kero hii mara nyingi,sasa lifanyieni kazi,”amesema Chongolo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *