Chongolo amfunda Makonda
DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amemuagiza Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid kufanya kazi kwa weledi na kusimamia misingi imara ya chama hicho.
Chongolo ametoa maagizo hayo baada ya Makonda na Rabia kufika ofisini kwake kujitambulisha na kuanza kazi, baada ya kukabidhiwa ofisi zao rasmi na watangulizi wao.
Chongolo amewataka viongozi hao wa Itikadi na Uenezi watambue majukumu yao, watambue imani kubwa waliyopewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, kutumikia Chama kupitia nafasi hizo walizoteuliwa.
“Nafasi mlizopewa ni moja ya maeneo ya kimkakati ya CCM, hivyo mnapaswa kujua kuteuliwa kwenu ni sehemu ya kuongeza chachu na kasi ya idara hizi kutekeleza malengo yaliyokusudiwa na CCM, katika kutumikia wananchi na kuzisimamia Serikali zote mbili za CCM.” Amesema Chongolo na kuongeza
“Karibuni sana. Hongereni sana kwa kuaminiwa na kuteuliwa. Ujio wenu utakuwa sehemu ya kuongeza kasi ya yale ambayo Chama tumekusudia. Uenezi na siasa ndiyo kila kitu. Mmeaminiwa na kuteuliwa kushika maeneo muhimu yatendeeni haki. ” Amesisitiza Chongolo
Aidha, amesema siasa na uhusiano wa Kimataifa ni mojawapo ya ‘core activities’ za chama hicho Tawala.
” Tunatarajia mtafanya makubwa kufikia malengo. Tuna maandalizi ya uchaguzi hapa, 2024 na 2025 uchaguzi wa serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu. Tuko kwenye reli…tuko kwenye track sahihi. karibuni sana.” Amesema Chongolo
Chongolo, pia alitumia nafasi hiyo kuwatakia kila la heri katika majukumu yao na kuwaelekeza kuwa, baada ya kukabidhiwa ofisi zao na majukumu yao rasmi na watangulizi wao, waanze kazi mara moja, kwa kuwa hakuna muda wa kusubiria.
Makonda na Rabia waliteiwa kushika nafasi hizo, hivi karibuni na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), iliyoketi katika kikao chake maalum chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 22, 2023, jijini Dodoma.