Chongolo amuonya mkandarasi umeme vijijini Moro

MKANDARASI anayesambaza umeme katika vijiji vya wilaya sita za mkoani Morogoro, Kampuni ya HNXJDL JV ya China amemkera Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo kwa kusuasua kukamilisha miradi hiyo kwa wananchi na kumtaka akajipange upya, vinginevyo sheria itumike kukatisha mkataba wake.

Chongolo ametoa kauli hiyo leo katika Kijiji cha Wami Dakawa, wakati akiendelea na ziara yake mkoani Morogoro kukagua na kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kuhamasisha uhai wa chama ngazi ya mashina na kuzungumza na makundi mbalimbali ya wananchi.

Wakitoa kero zao, wananchi hao walisema changamoto kubwa ni  wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini ni kusuasua kutekeleza kazi hizo kwa wakati na wengine wametelekeza miradi hiyo kwa kuacha nguzo bila kusambaza nyaya kwa muda mrefu.

Advertisement

Akizungumia hilo, Chongolo amesema kero hiyo iko maeneo mbalimbali nchini na haiwezi kuvumilika, hivyo kutaka mamlaka husika kuvunja mikataba ya wakandarasi kama hao na kuwapa wengine.

Awali Meneja wa Usimamizi wa Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Romanus Lwena amefafanua kuwa mkandarasi huyo alipewa shilingi Bilioni 47.5 kutekeleza mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili katika vijiji 60 vya wilaya sita mkoani humo.

Katika mradi wa kwanza Loti 16, wenye thamani ya Sh bilioni 26.6 unatekelezwa katika wilaya ya Kilombero,Kilosa na Gairo. Mradi huo kwa sasa umetekelezwa kwa asilimia 38 tu.

Aidha mradi wa pili ni Lot 17,unaotekelezwa katika vijiji vya wilaya tatu za Ulanga,Malinyi na Mvomero na hadi sasa ameshatekeleza kwa asilimia 27 tu.

“Ni kweli mkandarasi anasuasua na yuko nyuma tumeshamuandikia barua ya onyo na hatua itakayofuata kama hatajirekebisha ni kukatisha mkataba wake na kumpeleka kwenye mamlaka ya usajili ili imfutie leseni asifanya kazi popote nchini,”amesema Lwena.

Mkandarasi huyo alipewa zabuni hiyo Agosti  mwaka 2021 na kutakiwa kuukamilisha Februari 28,,mwaka huu na kuwa umebaki mwezi mmoja mradi ukamilike lakini kasi ya utekelezaji ni ndogo.

 

1 comments

Comments are closed.