KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amekemea mmomonyoko wa maadili katika jamii na kuwataka wazazi na walezi kusimamia malezi na kuitaka jamii iache kuiga na kukopa mila na desturi zisizo za utamaduni wa Mtanzania.
Kauli hiyo ameitoa leo wilayani Kilosa akiwa Kijiji cha Dumila Juu,alipotembelea na kuzungumza na wanashina namba 1, na wananchi katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuhamasisha uhai wa chama ngazi ya mashina.
Akiwa kijijini hapo wananchi walitoa kero na changamoto zao na ndipo akatumia pia nafasi hiyo kuwataka wazazi, walezi kusimamia maadili ya watoto na kuitaja jamii iache kuiga mila na desturi zisizo na maadili ya kitanzania.
“Simamieni maadili ya vijana wetu, endeleeni kuwalea watoto ,tuache kukopa mila na desturi ambazo ninaharibu mila zetu na sio kila jambo tunapaswa kuliiga,sio utamaduni wetu,” amesema Chongolo.
Awali baadhi ya wananchi wa eneo hilo wamesema vitendo vya ukatili wa kingono vinafanywa katika jamii dhidi ya watoto na kusema vinatekelezwa kwa kuiga tamaduni za nje ambazo sio maadili waka desturi za Mtanzania.