Chongolo ataka mabadiliko haraka mitaala ya elimu

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ameitaka serikali kuharakisha mchakato wa mabadiliko ya mitaala ya elimu itakayowawesha wahitimu wake wa ngazi mbalimbali kuwa na taaluma ya kujitegeme badala ya kuajiriwa.

“Tunataka mitaala itakayowajengea uwezo vijana na wahitimu wetu kwa ujumla kujiajiri kuliko kutegemea kuajiriwa,” Chongolo ameyasena hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Malangali, wilayani Mufindi.

Chongolo alisema mazingira ya sasa ya elimu nchini imewafanya baadhi ya wahitimu wakiwemo wa vyuo vikuu kuwa wategemezi badala ya wabobezi.

“Kama ni kilimo, biashara, uhandisi, udaktari na fani nyingine yoyote, tuwe na mitaala itakayoanza kuwaandaa vijana wetu toka ngazi ya chini kabisa kuwa wabobezi katika fani hizo,” alisema.

Alisema msimamo wa CCM ni kuwa na mitaala hiyo mipya na Rais Dk Samia Suluhu Hassan amekwishatoa kibali kwa Wizara ya Elimu kuja na mitaala hiyo haraka.

“Zamani katika shule zetu nyingi kilimo lilikuwa somo la lazima toka ngazi ya chini. Tuliopata bahati ya kusoma wakati wa mfumo huo tulijengewa msingi wa kuwa wajasiriamali hata kama hakuna ajira,” alisema.

Awali Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi, Dk Sophia Mjema aliitaka jamii kuwekeza nguvu kubwa itakayomuwezesha mtoto wa kike kufikia ndoto za elimu.

Pamoja na kuhakikisha maadili ya mtanzania na watoto wanalindwa pamoja na kupewa haki zao zote, Dk Mjema alisema watoto wa kike wakiendelezwa wanayo fursa ya kuwa viongozi wakuu kama ilivyo kwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan na kujiimarisha kiuchumi.

Katika mkutano wake huo wa siku ya pili ya ziara yake mkoani Iringa, Chongolo aliyeambatana pia na Katibu wa NEC Idara ya Oganaizesheni, Issa Haji Ussi (Gavu) alipokea taarifa, kero na maombi mbalimbali toka kwa wadau wa kata ya Malangali na kuzipatia ufumbuzi.

Amechangia Sh Milioni nne kati ya Sh Milioni 9.7 kukamilisha ujenzi  wa msikiti wa Malangali huku Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini David Kihenzile akichangia Sh Milioni tatu, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Leonard Mahenda akichangia Sh Milioni mbili na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego  Sh 700,000.

Aidha amejibu ombi la Kihenzile kuhusu barabara ya Mbalamaziwa Malangali linalotaka ijengwe kwa kiwango cha changarawe akimtaka Mkuu wa Mkoa kufuatilia taarifa za ujenzi huo na kuzifikisha kwake ili azifanyie kazi.

Chongolo ameahidi pia kukitafutia kituo cha afya Malangali gari la wagonjwa pamoja na mashine ya mionzi (X ray)- aliyoahidi kuileta mara baada ya halmashauri ya wilaya ya Mufindi kujenga chumba kwa ajili ya huduma hiyo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwambia wananchi wa kata hiyo kwamba serikali imetoa zaidi ya Sh Milioni 600 kwa shule ya sekondari Malangali kwa ajili ya ukarabati wa hosteli za wanafunzi.

Habari Zifananazo

Back to top button