Chongolo: Msiuze chakula kikiwa shambani

Chongolo: Msiuze chakula kikiwa shambani

WANANCHI wilayani Kiteto mkoani Manyara, wameaswa kuacha kuuza mazao yakiwa shambani kwa bei ndogo na kisha baadaye kuja kuyanunua kwa bei kubwa kutoka kwa walanguzi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo katika mkutano na wananchi mjini hapo na kuwaonya kuwa njaa iliyopo sasa inachangiwa na wao kutoweka akiba, ilihali wilaya hiyo ni moja ya maeneo yanayozalisha mahindi kwa wingi nchini.

“Acheni kuuza chakula kikiwa shambani, hapa Matai na Kiteto yote mnazalisha mahindi kwa wingi, leo kuna njaa na mmeomba mletewe chakula cha njaa, sasa acheni kuuza chote, muwe mnaweka akiba,” amesema Chongolo.

Advertisement

Kiteto ni miongoni mwa wilaya zinazokabiliwa na njaa na tayari Wakala wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA),amekiri kuwepo na uhitaji wa chakula na tayari tani 32 za mahindi zimeshawasili na kilo moja itauzwa kwa shilingi 700 badala ya bei ya awali ya shilingi 880.