Kairuki azindua mkakati zao la mianzi

Waziri Kairuki

DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki amekitaka Chuo cha Viwanda vya Misitu Moshi kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo ( SIDO )na wadau wengine kutafuta teknolojia ya kisasa na rahisi ya kuchakata mazao ya mianzi ili kuziongezea viwango vya thamani bidhaa za zao hilo.

Waziri Kairuki ametoa agizo hilo leo Februari 19, 2024, katika uzinduzi wa Mkakati wa Kitaifa wa Mianzi na Mpango kazi wa mwaka 2023/2031 wenye kauli mbiu ya “Tanzania inawekeza katika Mianzi kwa ajili uchumi endelevu” uliofanyika katika Chuo cha Taifa cha Utalii jijini Dar es Salaam.

Mkakati huo unatarijiwa kuongeza pato la taifa, kuingiza fedha za kigeni pamoja na kutatua tatizo la ajira huku ukisaidia matumizi ya mahitaji ya kijamii na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi ikiwemo mmonyoko wa ardhi.

Advertisement

Aidha, Waziri Kairuki ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Misitu kufanya tafiti za kutambua maeneo sahihi ya kupanda aina mbalimbali ya mbegu za Mianzi, huku akiwataka Wakala wa Huduma za Misitu nchini kurahisisha upatikanaji wa mbegu za mianzi kwa wadau na wananchi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya ya Bunge ya Ardhi, Maliasiali na Utalii Timotheo Mnzava , amesema mianzi ni zao muhimu katika uchumi lakini umuhimu wake haujulikani kwa watu wengi.

Mkurugenzi wa Shirika la Mianzi Duniani ( INBAR) Ali Mchumo, amesema biashara ya mianzi duniani ina ukubwa wa dola Milioni 70, huku akiiomba Serikali kutoa elimu endelevu kwa wananchi juu ya umuhimu wa mianzi.

Akiwakilisha wakuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo, amemuhakikishia waziri kuilinda, kupanda na kutoa elimu ya zao hilo la kimkakati kwa wananchi katika halmashauri na wilaya zao.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hassan Abbasi ameahidi kutekeleza mkakati huo na maelekezo yatolewayo na kuendelezwa.