CHUO Kikuu Mzumbe kilichopo mkoani Morogoro, kimezindua ofisi maalumu ya dawati ya jinsia, ili kutimiza malengo ya serikali ya kupunguza na kumaliza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika vyuo vikuu na kwenye jamii nchini.
Hatua ya uzinduzi wa ofisi ya dawati hilo ni utekelezaji wa agizo la serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum kwa lengo la madawati hayo kuwa na majukumu ya kutokomeza aina zote za ukatili maeneo ya vyuo.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Profesa William Mwegoha, amesema hayo Machi 23,2023 chuoni hapo kwenye hotuba yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Fatma Mwassa kwenye uzinduzi dawati hilo kampasi kuu ya Morogoro. Mkuu wa Mkoa aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa.
Profesa Mwegoha amesema uongozi wa chuo hicho umetoa jengo , kulikarabati na ununuzi wa vifaa kwa ajili ya matumizi ya wajumbe walioteuliwa wa dawati hilo, ambalo litafanya kazi kwa kuzingatia mwongozo wa serikali.
Ametaja njia zitakazotumika kupata taarifa za unyanyasaji wa kijinsia ni pamoja na mlengwa kufika moja kwa moja kwenye ofisi za dawati la jinsia, kupiga simu kupitia namba ya wazi ambayo mtu yeyote anaweza kupiga na kutoa taarifa zake kwa njia ya barua pepe na kutumia sanduku la maoni.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Morogoro , Nsemwa kwa niaba ya mkuu wa mkoa amesema, hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la matukio yanayohusiana na unyanyasaji wa kinsia na mashambulio ya aibu yanayohusisha wana familia na jamii kwa ujumla.
Amesema dawati hilo la jinsia liwe chachu kutokomeza ukatili wa jinsia chuoni, huku akiwataka wajumbe wa dawati hilo kutunza siri na kutoa msaada unaostahili kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia, ili kujenga jamii iliyo bora.