Manchester City na Arsenal leo zitashuka Uwanja wa Etihad katika mchezo wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England ‘EPL’, mchezo utakaopigwa saa 4:00 usiku.
‘The Gunners’ wanaongoza ligi hiyo kwa pointi tano, lakini wako mbele kwa michezo miwili zaidi dhidi ya mabingwa watetezi wa Pep Guardiola.
Pande zote mbili zinatambua kuwa ushindi wa leo utawafanya wachukue udhibiti wa mbio za ubingwa huku ikiwa imebaki michezo mitano kwa Arsenal na saba kwa City.
Arsenal ya Mikel Arteta, ambayo ilikuwa nyuma kwa pointi nane mwanzoni mwa mwezi, ilishinda taji hilo mara ya mwisho mnamo 2003-04, chini ya kocha Arsene Wenger.
Wakiwinda taji la tano la Premier League ndani ya miaka sita, City pia wako kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Kombe la FA na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Arteta amesema kuwa anaamini mchezo huo hautaamua bingwa wa EPL msimu huu kwani kwa upande wake anaangalia zaidi michezo mitano iliyobaki na ndiyo itaambua hatma ya Arsenal msimu huu.
Kwa upande wa Guardiola amesema kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kutokana na ubora wa mpinzani wake na kuongeza kuwa licha ya City kuwa na matokeo ya ushindi dhidi ya Arsenal kwenye michezo ya miaka ya karibuni ila historia haichezi.
Arsenal inaongoza ligi ikiwa na pointi 75 akifuatiwa na City mwenye 70, huku ikiwa na michezo miwili mkononi.