COP28 ‘jicho’ la Tanzania

kuinuka uwekezaji kimataifa

MKUTANO wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP28) unatarajiwa kufanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 12, 2023 ambapo washiriki zaidi ya 80,000 wanatarajiwa kuhudhuria.

Lengo la mkataba huo ni kuongeza juhudi kupunguza ongezeko la gesijoto katika anga linalotokana na shughuli za binadamu ili lisifikie katika kiwango chenye athari kubwa kwa binadamu na mazingira na kuziwezesha nchi wanachama kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mabadiliko ya tabianchi ni suala lenye changamoto nyingi duniani kutokana na athari zake kiuchumi, mazingira, utamaduni na kijamii.

Tanzania ni Mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC). Mwaka 2022 Tanzania ilishiriki mkutano wa 27 (COP27) nchini Misri na kupata mafanikio makubwa kama nchi.

Mafanikio COP27 na ushiriki wa Tanzania COP28

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo akizungumza kuhusu ushiriki na msimamo wa Tanzania kwenye COP28 anasema miongoni mwa manufaa yaliyopatikana COP27 ni uanzishwaji wa miradi ya nishati jadidifu ambayo itafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa Dola za Marekani bilioni 18, Taasisi ya Afrika 50 na Shirika la Nishati la Afrika kwa kushirikiana na kampuni ya China Renewable Energies.

Anasema tayari Wizara ya Nishati imeshakamilisha na kusaini mikataba na taasisi ya kampuni ya Equinor na ya TAQA Arabia Septemba 5, 2023 ambapo Tanzania imeasaini Hati ya Makubaliano ya Mashirikiano na Serikali ya Norway kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

“Pia Shirika la 2050 Pathways limekubali kusaidia Tanzania kuandaa mkakati wa upunguzaji gesijoto na Shirika la Uhifadhi la Kimataifa (TNC) limefadhili tathmini ya awali kwa ajili ya kuandaa Mpango wa Matumizi ya Bahari. Tanzania imejiunga na taasisi zinazoshughulika na mabadiliko ya tabianchi,” anaeleza Dk Jafo.

Anasema kutokana na mafanikio hayo waliyoyapata katika mkutano wa 27,  kwa mwaka huu wamejipanga vizuri zaidi kuelekea katika ushiriki wa mkutano wa 28 ambapo Ujumbe wa Tanzania unatarajia kuongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Msimamo wa Tanzania COP28

Katika kuwezesha ushiriki wenye tija, Tanzania imeandaa Msimamo wa Nchi kwa ajili ya kulinda na kutetea maslahi ya taifa katika majadiliano yatakayofanyika katika mkutano huo.

Dk Jafo anabainisha msimamo huo umeandaliwa kwa kuzingatia sera, mipango na mikakati ya taifa, pamoja na ushirikiano na makundi ya nchi.

“Mkutano wa COP28 umetanguliwa na mikutano mingine ya kikanda na kimataifa ya uwili, mikutano hiyo inalenga kuziandaa nchi na makundi husika kuwa na misimamo ya pamoja kuhusu ajenda na mada zitakazojadiliwa wakati wa mkutano ambapo tutaweka bayana msimamo wake pamoja na kushawishi nchi na makundi husika kuunga mkono msimamo wetu.

Pamoja na hayo anasema Tanzania imepanga kuendesha mkutano mkubwa wa pembezoni ambao utawaleta pamoja wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa ya Afrika na mabara mengine, sekta binafsi, wafanyabiashara, taasisi zisizo za serikali, mashirika ya Umoja wa Mataifa na taasisi za fedha na washirika wa maendeleo.

Anasema lengo la mkutano huo ni kuwaleta pamoja wadau wote na kuvutia wawekezaji katika fursa za mabadiliko ya tabianchi zilizopo nchini.

Pia anafafanua mkutano huo unalenga kuongeza chachu ya uwekezaji wa kimataifa kwa kutumia fursa katika sekta kwa kuvutia wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani kufahamu fursa za uwekezaji zilizopo na zinazopatikana nchini.

Dk Jafo anasema na mkutano mkuu wa COP28, kutakuwa na mikutano mingine itakayohusisha viongozi na wataalamu ambayo huandaliwa na nchi au taasisi husika ambapo katika mikutano hiyo Rais Samia atakutana na viongozi na wakuu wa nchi na mashirika ya kimataifa.

Anasema lengo la Mikutano ya Uwili ni kusaidia nchi kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga uwezo wa nchi kuhusu masuala ya hifadhi ya mazingira kwenye sekta ya kilimo, uvuvi, uchumi wa buluu, nishati, na udhibiti wa taka za plastiki.

“Pamoja na kuiwezesha nchi kupata fursa ya nafasi za vijana katika mafunzo kwa vitendo kwenye Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi na fursa ya upatikanaji wa ajira kwa vijana.

Aidha, lengo lingine analoliainisha ni kusaidia nchi kupata ajira, kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kujenga uwezo wa nchi kuhusu masuala ya hifadhi ya mazingira.

Mkutano huu wa COP28 ni sehemu muhimu kusaidia nchi yetu kupata, kuandaa na kutekeleza miradi ya kukabiliana na majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, kupata fursa za mafunzo na ajira kwa vijana katika ngazi za kimataifa,” anasisitiza.

Anasema kupitia mkutano huo Tanzania itajitangaza kimataifa kupata fursa za uwekezaji.

Fursa kwa Watanzania

Ofisa Misitu Mkuu, Dk Frendrick Manyika anaiambia HabariLEO kuwa kuelekea mkutano wa COP28 Tanzania ina vipaumbele 22 ambavyo vinaingiliana ikiwemo matumizi ya nishati safi inayotokana na mimea, wanyama (biogas), gesi asilia, gesi oevu, majiko banifu, nishati ya umeme, mkaa mbadala na majiko yanayotumia nishati ya jua kwani nishati safi inasaidia kupunguza uzalishaji wa gesijoto ikiwemo hewa ya kaboni.

Dk Manyika anasema vipaumbele vingine ni kilimo endelevu, biashara ya kaboni, uchumi wa buluu.

“Na pia kuna masuala la udhibiti na upotevu wa mali, upatikanaji wa fedha za kushughulikia athari za mabadiliko ya tabianchi na inatakiwa kupatikana kwa wakati, kufanyika kwa tafiti za kukabiliana na mabadiliko na teknolojia,” anaeleza.

Anasema Watanzania wanatakiwa wasione mabadiliko ya tabianchi kwa upande hasi tu bali watumie nafasi hizo katika kufanya kazi na ubunifu na teknolojia na kufanya tafiti wapate faida na kuimarisha vipato.

“Mbali ya kuwa kuna changamoto hasi zinazojitokeza lakini ni muhimu kutumia changamoto kama fursa mfano kuna watu wanafanya shughuli za za kibunifu za kutengeneza teknolojia ambazo zinakuwa rafiki kwa mazingira, utengenezaji wa nishati safi unaweza kuwa sehemu ya kujiajiri pia.

Fursa nyingine anasema ni kutumia biashara ya kupunguza hewa ukaa ijulikanayo kama soko la kaboni na kutaka Watanzania watumie fursa hizo kwani zinaweza kuwaingizia kipato na tayari vikundi vingine wameshaanza kupata faida katika vijiji, kata, wilaya na mikoa hivyo ni muhimu kutafuta fursa na kufanyia kazi kuleta ustahimilivu wa athari za mabadiliko ya tabianchi.

Makala haya yamewezeshwa na Mesha na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.

 

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button