RAIS wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa janga la Covid 19, vita barani ulaya na mabadiliko ya tabianchi vimeipa somo serikali na inajipanga vizuri kuhakikisha inakuwa na akiba ya chakula cha kutosha.
Rais Samia amesema hayo leo June 13, 2023 jijini Mwanza alipokuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la Utamaduni la Bulabo linaloendelea katika Uwanja wa Red Cross Ngomeni Kisesa jijini humo.
Amesema, kutokana na sababu hizo tatu hatua stahiki tayari zimeshachukuliwa za kuongeza matumizi katika sekta ya kilimo ili watu wavune zaidi na Taifa kuwa na akiba ya kutosha ya chakula.
Amesema, serikali ina mpango wa kusajili wakulima ili iwatambue ni watu wangapi wanajishughulisha na sekta hiyo ili ijipange vizuri.
“Ndio maana mbolea za ruzuku zimeanza kutolewa ingawa kuna changamoto za hapa na pale kwenye ugawaji wake, tunajitaidi kukabiliana nazo ili ziweze kuwafikia wakulima kwa urahisi.”Amesema Rais Samia
Aidha amesema, fedha nyingi tayari zimeshatengwa kujenga ‘scheme’ za umwagiliaji ili wakulima wawe na misimu miwili ya mavuno kwa mwaka.
Amesema, serikali ina mpango wa kujenga maghala katika kila mkoa yatakayokuwa katika mfumo wa Kanzi Data kwa dhumuni la kubaini kila ghala lina kiasi gani cha chakula ili tatizo linapotokea kuwe na uhakika wa kuwahudumia wananchi.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema kuwa tayari ameshatoa maagizo kwa Waziri wa Fedha na Kilimo waanze na ununuzi wa mazao msimu huu wa mavuno ili nchi iwe na chakula cha kutosha, huku akiwataka wakulima kutokuuza mazao nje ya nchi kwa kuwa Serikali itayanunua.