MNYORORO wa thamani wa kilimo cha muhogo wilayani Handeni mkoani Tanga unatarajia kuongezeka baada ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) kujenga kiwanda cha kuchakata zao hilo katika kijiji cha Pachaga, Mkata.
Kaimu Mkurugenzi wa CPB, John Maige alisema kiwanda hicho ni kati ya viwanda 25 vinavyotarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini yanayozalisha muhogo kwa wingi vinavyotarajiwa kuanzishwa na bodi yao.
Ametoa taarifa hiyo leo mjini Iringa wakati akiwasilisha mada kuhusu bodi hiyo na majukumu yake katika semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari juu ya shughuli za bodi hiyo.
Alisema kiwanda hicho kitakachokuwa na uwezo wa kuajiri wafanyakazi watano wa kudumu na wengine 80 wa muda kitakuwa na uwezo wa kuchakata tani 12 za muhogo kwa siku.
“Kiwanda hicho kilichojengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 300 kipo katika hatua za mwisho kukamilika; Juni 19, mwaka huu mashine zitaanza kufungwa kazi itakayokamilika kwa muda siku saba na mwezi Julai kiwanda kinatarajiwa kuanza kufanya kazi,” alisema.
Alisema wameanza na wilaya ya Handeni kwa kuwa wanatambua uwepo wa zaidi ya wakulima 6,000 wa zao hilo na namna serikali chini ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Godwin Gondwe alivyohamasisha kilimo hicho.
Akizungumzia majukumu ya bodi hiyo kufanya biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko na kushirikiana na wadau wengine kuongeza thamani ya mazao hayo, Maige alisema; “Mbali na kuuza bidhaa hizo ndani na nje ya nchi, bodi yetu inawajibu pia wa kuagiza vyakula kutoka nje na kuuza kwa wananchi kwa bei nafuu pale mahitaji yanapoongezeka tofauti na kile tulichonacho ndani.”
Aliwataka wahariri kuwaelimisha wakulima kuzalisha kwa kuzingatia ubora na mahitaji ya soko ili wafikapo sokoni, bidhaa zao zisipate changamoto ya ukosefu wa soko.
Alizitaja huduma zingine zinazoambatana na utekelezaji jukumu la biashara kuwa ni pamoja uhifadhi wa mazao, usagishaji wa nafaka, usafirishaji na upangaji wa madaraja ya mazao ya nafaka na huduma ya mzani.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Biashara na Masoko, Evans Mwanibingo alisema CPB imeanza utekelezaji wa majukumu yake msimu wa 2015/2016 kwa kufufua kiwanda cha kuzalisha unga cha Iringa na imekuwa ikiongeza viwanda kwa kadri uwezo wa kifedha unavyoongezeka.
“Toka wakati huo CPB imekiwa ikinunua mazao mbalimbali kutoka kwa wakulima kwa ajili ya malighafi ya viwanda vyake na biashara,” alisema.
Alisema ununuzi wa nafaka na mazao mchanganyiko kuanzia mwaka 2019/ 2020 umeongezeka kutoka tani 31,585 hadi tani 51,538 mwaka 2021/2022.
Katika kuongeza thamani alisema mwaka 2020/2021 tani 5,632 za mahindi na alizeti zilichakatwa huku tani 14,623 za mahindi, alizeti, mpunga, mafuta ghafi na ngano zikichakatwa mwaka 2021/2022.
“Katika kuchakata mazao hayo bado CPB haijafikia asilimia 30 na lengo letu ni kihakikisha tunafika asilimia 80 sambamba na kuongeza ununuzi wa nafaka na mazao mchanganyiko,” alisema.