CRB kukagua miradi wakandarasi wa kigeni

ARUSHA;  BODI ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imesema inaanza operesheni maalumu kukagua miradi mikubwa inayotekelezwa na wakandarasi kutoka nje ya nchi, kutokana na miradi mingi kutekelezwa chini ya viwango.

Imebaini hayo kufuatia ziara mbalimbali za Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa katika miradi mbalimbali, ikiwemo barabara ambayo imeonekana thamani yake kuwa ndogo.

Akizungumza leo jijini Arusha, katika mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa wakandarasi, Msajili wa CRB, Rhoben Nkori, amesema bodi hiyo imeamua kufanya operesheni hiyo maalum kuanzia mwezi Mei hadi katikati ya mwezi Juni mwaka huu.

Advertisement

Amewataka wakandarasi wote kutambua kuwa operesheni hiyo maalum itafanyika hadi mwezi Juni, 2024 kujiridhisha wakandarasi wote walioingia mkataba na serikali kama wanafanya kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na sheria, kinyume na hapo hatua zitachukuliwa.

“Bodi imeamua kufanya operesheni maalum ya kutembelea miradi na kukagua miradi yote mikubwa inayofanywa na wakandarasi wa nje kwa sababu miradi mingi mikubwa inafanywa na wakandarasi wa nje,”amesema.

“Na hili limetokana na tumefuatilia ziara za Waziri wa ujenzi amepita katika miradi mingi ya barabaraa ambayo tunaona miradi ambayo wakandarasi wa nje kwenye miradi hii mikubwa inatekelezwa tofauti na ambavyo bodi inategemea, kwani tulitegemea wakandarasi ni wakubwa na wanafanya miradi kama walivyoingia mikataba na kwa muda unaotakiwa,” Amesema na kuongeza:

“Baada ya kufuatilia ziara ya Waziri tumeamua kama bodi kupitia miradi hii na kujifunza utekelezaji thabiti kwa wakandarasi waliofanya vizuri ili kujifunza mbinu walizotumia, ili zisaidie kutumia kwa wakandarasi wazawa.

“Kikubwa zaidi kwenda kupitia na kuangalia wakandarasi hawa ambao wanafanya kazi kwa kusuasua na tumewasajili wakiwa ni wakandarasi wakubwa ni kwa nini wanafanya miradi chini ya kiwango au kufanya kinyume na tutakagua tukijiridhishisha wakandarasi hawa kazi wanazofanya haziendani na mikataba waliyoingia na kama sheria yetu itaturuhusu kuchukua hatua kwa kuwaondoa kwenye usajili kama ambavyo tuliwaingiza,”alisema.

Meneja wa CRB Kanda ya Kaskazini, Sauda Njila alisema mafunzo hayo ya siku tatu yatakutanisha wadau 150, ambapo mafunzo hayo ya usimamizi wa fedha yatasaidia sekta hiyo ya ujenzi hapa nchini hasa wa wakandarasi wazawa.

Amesema mafunzo hayo hutolewa kufuatia tafiti mbalimbali ambapo wamebaini Makandarasi wakipata mafunzo mbalimbali yatawasaidia kuboresha utendaji kazi wao na kuwa na matokeo mazuri.

Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makandarasi na watoa huduma ShirikishiTanzania (TUCASA), Mhandisi Yahaya Mnali, amesema mafunzo hayo ni muhimu na yana manufaa kwani yatasaidia kuboresha fani hiyo na
kutekeleza wajibu wao kikamilifu.

“Kabla ya mafunzo haya inawezekana kazi zilikuwa zinafanyika, matokeo yake zinaonekana dosari za hapa na pale labda zilitokana na kutofahamu masuala mengine ikiwemo usimamizi wa fedha na sisi wakifanya kazi kwa ubora wataaminiwa na watakuwa na uwezo wa kufanya kazi kubwa na tutakuza uchumi wetu,”amesema