CWT yashauri ajira zaidi kwa walimu

CHAMA Cha Walimu Tanzania (CWT) kimeiomba serikali iendelee kuajiri walimu ili kuwe na uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45 tofauti na sasa ambapo uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi ni 66

Katibu Mkuu wa CWT, Japhet Maganga alisema hayo juzi wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho. Alisema kuwa taifa sasa lina walimu 274,901. Walimu wa shule za msingi wakiwa 185,401 na walimu wa shule za sekondari 89,500.

Idadi ya wanafunzi wa shule za msingi ni 12,325,130 na hivyo kufanya uwiano wa sasa kuwa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 66 kwa shule za msingi.
Alisema kiwango hiki bado ni cha juu ikilinganishwa na kiwango ambacho wizara imepanga taifa kufikia uwiano 1:45 .

“Ili tuweze kufikia lengo hilo , Chama cha Walimu Tanzania tunaendelea kuiomba serikali kuajiri walimu wengine kwani bado mahitaji ni makubwa sana,”_alisema.

Wakati huo huo aliomba serikali izitake benki mbalimbali kushusha kiwango cha riba kinachotozwa katika mikopo ili kuwapa unafuu walimu na watumishi wengine kutojiingiza katika mikopo inayowafedhehesha, .

“Kuwekwe utaratibu mzuri wa kuwakopesha watumishi wa umma ardhi wakiwamo walimu hususani katika mamlaka za serikali za mitaa ili walimu waweze kukopa na kuweza kujiandaa vema kustaafu kwa heshima,” alisema.

Aliipongeza serikali kwa kuanza mchakato wa kuboresha na kupitia mitaala ya elimu ya awali na msingi ili kuboresha elimu nchini.

Alishauri mchakato uwe mpana na wa muda wa kutosha bila kusahau kuwashirikisha wadau wote na hasa walimu katika hatua zote.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Makamu wa Rais, DkPhilip Mpango, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako alikemea udangangifu wa mitihani unaofanywa na baadhi ya watumishi wa serikali wasio waaminifu.

Aliwataka wakuu wa shule kutojiingiza katika udanganyifu huo. Vile vile alisema serikali inazifanyia kazi changamoto zote zinazowakabili walimu.

Habari Zifananazo

Back to top button