DAKTARI bingwa wa magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) amesema ndani ya dakika tatu mtu anaweza kuokoa maisha ya mtu ambaye moyo wake umesimama ghafla akaendelea kuishi.
Dk Khuzeima Khanbhai alisema miongoni mwa vyanzo vya moyo kusimama ni matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, mishipa ya damu kuziba, mtindo wa maisha ukiwamo unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara.
“Kuna mtu anatatizo la mfumo wa umeme wa moyo ambao ni ama wa juu au wa chini ikiwa na maana moyo kudunda haraka isivyo kawaida au kudunda polepole isivyo kawaida, uwezekano wa kupata tatizo la moyo kusimama ni mkubwa,”alisema Dk Khuzeima na kuongeza;
“Moyo ukiwa na shida yoyote iwe ya kutanuka kutokana na unywaji wa pombe, mishipa kuziba, na mtindo mbaya wa maisha ambao ni pamoja na lishe mbaya na vyakula vya mafuta mengi, unaongeza uwezekano wa moyo kusimama ghafla”.
Alisema unaweza kuokoa maisha ya mgonjwa kwenye tatizo hilo ndani ya dakika tatu tangu hali hiyo itokee kwa kumlaza chali na kuanza kumpa huduma ya kwanza ya kuushtua moyo kwa kukandamiza kifua kwa kutumia mikono ili uendelee kufanya kazi.
“Huduma ya kwanza ya kuufufua moyo na mapafu (CPR), imeonesha inapofanywa kwa usahihi kwa mgonjwa, unaokoa maisha ya mgonjwa kwa asilimia zaidi ya 95 ndani ya muda sahihi mara tu baada ya mtu kupata tatizo hilo,”alisema Dk Khuzeima.
Alisema huduma ya kwanza ya CPR inastahili kufundishwa kuanzia shuleni hadi nyumbani ili watu wengi wafahamu namna ya kumsaidia mgonjwa kuokoa maisha yake.
Dk Khuzeima alisema moyo unaposimama ghafla ina maana damu inakuwa haipelekwi kwenye maeneo yake ikiwemo kwenye ubongo, mapafu na maeneo mengine hivyo mgonjwa anapofanyiwa CPR husaidia kuushtua na damu itaendelea kutembea hivyo anaweza kupona.
Alisema utafiti wa madaktari wa Marekani mwaka 2017 ulionesha kati ya watu 100,000 watu 74 wanapata tatizo la moyo kusimama ghafla nje ya hospitalini na kati ya watu saba mmoja anafariki dunia kwa tatizo hilo.
Alitaja dalili za mtu kupata tatizo hilo ni sekunde chache kabla ya moyo kusimama ghafla ni kizunguzungu, kifua kuuma ghafla, pumzi kubana au kusikia kichefuchefu.
Akizungumzia namna unywaji pombe na uvutaji sigara unavyochangia maradhi ya moyo kwa vijana alisema kuna utafiti waliufanya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Tawi la Mloganzila mwaka 2019/2020.
Dk Khuzeima alisema matokeo ya utafiti huo yalionesha kuwa vijana wengi hivi sasa wanapata kiharusi kuliko wazee kwa kuwa wana shinikizo la juu la damu.