WANAUME wenye umri wa kuanzia miaka 40 na kuendelea wameshauriwa kujenga utamaduni wa kupima saratani ya tezi dume mara kwa mara ili wale wanaobainika kuwa na matatizo wapate matibabu mapema.
Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi wa Hospitali ya KAM Musika ya mkoani Dar es Salaam, Dk Kandore Musika. Hospitali hiyo iliandaa kambi ya bure ya kupima wanaume dalili za tezi dume.
Dk Musika alisema iwapo mtu atabainika mapema kuwa na dalili za saratani ya tezi dume, inakuwa rahisi kwake kupata matibabu na kupona kuliko kusubiri mpaka saratani ifikie hatua mbaya.
Alisema wameamua kuandaa kambi hiyo ya bure ya siku moja kuwapa fursa wananchi wa maeneo ya Kimara ilipo hospitali hiyo, kupima saratani ya tezi dume na wale watakaobainika kuwa na tatizo hilo waanzishiwe matibabu mapema.
“Ugonjwa wa saratani ya tezi dume unawashambulia sana wanaume wenye miaka kuanzia 40 na kuendelea na hospitali ya KAM imeamua huduma hii bure kama shukrani kwa jamii inayotuzunguka,” alisema Dk Musika.
Alisema wanaume wengi hawana uelewa kuhusu saratani ya tezi dume hivyo wamelazimika kuwaelimisha kuhusu dalili zake ili waweze kuwahi hospitali watakapoziona.
Dk Musika alisema mamia ya wanaume waliojitokeza kwenye kambi hiyo ya bure wamepewa somo la kutosha kuhusu dalili za ugonjwa huo na wameahidi kwenda kuelimisha wenzao.
“Mtu mwenye saratani ya tezi dume akichelewa akikaa nayo muda mrefu matokeo yake inasambaa mwili mzima na kushambulia kila sehemu kwa hiyo kupima mara kwa mara si jambo la kupuuza kwa wanaume watu wazima,” alisema.
“Hatutaishia kupima saratani ya tezi dume tu, tutafanya utaratibu wa kupima bure saratani ya matiti na saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake kama sehemu ya kutoa shukrani kwa jamii tunayoihudumia,” alisema Dk Musika.
John Rwekaza (80), ambaye alipimwa saratani ya tezi dume aliishukuru hospitali hiyo kwa uamuzi wake wa kutoa huduma hiyo bure kwani wazee wengi hawana uwezo wa kwenda kupata vipimo hivyo.