Daktari: Dawa kutuliza maumivu hatari kwa figo

DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam, Immaculate Goima amesema matumizi ya dawa za kutuliza maumivu na dawa mbadala yanachangia kusababisha magonjwa ya figo.

Akizungumza katika mahojiano na HabariLEO jijini Dar es Salaam jana, Dk Goima aliishauri jamii iache kutumia dawa bila ushauri wa wataalamu.

“Watu wanatumia madawa hovyo, hasa dawa za kutuliza maumivu na pia kuna baadhi ya sehemu kutokana na mila na desturi zetu watu wanatumia sana mitishamba ambayo hatujui usalama na kipimo chake na inasababisha kuathiri figo,” alisema na kuongeza:

Advertisement

“Kibaya ni kwamba magonjwa ya figo yanakuwa hayana dalili mpaka dalili zionekane, anakuwa ameshafikia hatua ya mwisho kwa sababu kwa hatua ya kwanza, pili na tatu hakuna dalili na ikishafika nne na tano ndio dalili zinaanza.”

Dk Goima alisema dalili za juu za kuharibika figo ni mkojo kupungua, kuvimba uso, miguu kujaa, kutapika na upungufu wa damu kwa sababu asilimia 25 ya damu inatengenezwa na figo.

Daktari Bingwa wa Upasuaji, Mfumo wa Mkojo na Figo katika MNH –Mloganzila, Hamisi Isack alisema tatizo la figo linasababishwa na vitu vingi.

“Ugonjwa wa figo wa kudumu au wa muda mrefu ni tatizo ambalo linaathiri watu wengi duniani na kutokana na tafiti zilizofanywa ndani ya nchi hii, inaonesha kwamba kati ya asilimia saba hadi 15 ya Watanzania, wameathrika na ugonjwa wa figo,” alisema Dk Isack na kuongeza:

“Kuna shinikizo la damu, maradhi ya kuambukiza kama HIV, homa ya ini na kuna maradhi ambayo yanasumbua figo moja kwa moja na wakati mwingine chanzo kinaweza kisijulikane kwa tafiti duniani hadi asilimia 20 na hapa kwetu mpaka asilimia 49 kipindi ambacho mgonjwa amefikia matibabu ya figo.”

Dk Isack alisema matibabu sahihi ya kupona kabisa ni kupandikiza figo na usafishaji ni kama njia ya kuelekea kupandikiza mazingira yanaporuhusu.

“Kiasi cha chini kupata matibabu ya kupandikiza figo nje ya nchi ni Sh milioni 100 na sasa hapa kwetu huduma zinapatikana kwa milioni 30 tu,” alisema.

/* */