Daktari: Kichaa cha mimba si ushirikina, kinatibika hospitali

Kichaa cha mimba si ushirikina, kinatibika hospitali

KICHAA cha mimba ni msongo wa mawazo unaowapata kina mama baada ya kujifungua.

Kahabi Mathias (22) mkazi wa Kijiji cha Kagera, Kata ya Nyankede, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, Shinyanga  amepatwa na kichaa cha mimba baada ya kujifungua kwa upasuaji na mtoto kufariki.

Kahabi mwenye watoto wawili na huyo aliyefariki alikuwa wa tatu, amelazwa katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama kwa kipindi cha wiki moja sasa kutokana na tatizo la kichaa cha mimba.

Advertisement

Mama mkwe wake anayeitwa Monika Ntolwa anayemuuguza hospitalini hapo anaeleza kuwa alipokuwa anaumwa uchungu walimpeleka kwenye zahanati hali ikawa mbaya wakapewa rufaa kwenda Kituo cha Afya cha Bulungwa.

“Tulipofika kituo cha afya uchungu nao umekazana daktari kuona hali ni mbaya wakamfanyia upasuaji wa haraka kwani mtoto tayari alikuwa amekwisha fia tumboni wakamwokoa mama,” anasema Monika.

Monika anasema waliporuhusiwa kurudi nyumbani alikuwa mzima na mtoto walipewa familia ikamzika Kahabi akishuhudia nyuma ya nyumba kama utamaduni wa Wasukuma unavyoeleza.

“Walichoshangaa mama huyo alichukua jembe kimyakimya nakwenda eneo ambalo wamefukia mwili wa mtoto huyo  nakuanza kumfukua walipo muona walimnyang’anya jembe na kumhoji alieleza anataka kumnyonyesha mwanaye,” anasema  Monika.

Anasema walipomrudisha hospitalini daktari aliwaeleza huenda ana malaria lakini aliwapa rufaa kwenda Hospitali ya Manispaa ya Kahama ambapo amelazwa kwa wiki sasa na hali yake kiakili bado haijawa sawa.

“Vituko ambavyo amekuwa akivifanya anachukua chupa kubwa za maji nakutaka kubeba mgogoni wakati mwingine anachukua nguo anazikusanya  nakutoa ziwa kama anataka kunyonyesha mtoto,” anasema Monika.

Anasema hospitalini hapo imebidi watengwe kwenye wodi yao kwa kuwa anapiga watu. Sasa analindwa na wanaume watatu akiwepo mume wake ili kuzuia fujo anazofanya.

Anaeleza kuwa alitoroka wodini na kwenda kwenye wodi ya watoto wachanga aliposikia sauti ya kulia huku akisema wampe mtoto wake anyonye kwani amesikia analia.

Mjomba wa Kahabi, Shija Masalu anasema kuwa amekuwa na nguvu za ajabu kwani wanawake wanashindwa kulala naye wodini anawashinda nguvu na kuwapiga, anaishi kwa juisi na maji na akipewa chakula anakataa kula.

Winga Masalu mzazi wa Kahabi anasema alimzaa mwaka 2000 na alipofikisha miaka 14 alimuozesha na sasa ana watoto wawili na mtoto aliyefariki ni wa tatu. Mtoto wa kwanza ana miaka mitano.

“Hospitalini hapa wamekuwa wakimpatia dawa ya sindano ya kulala hata saa nne mfululizo lakini akiamka hali inarudi tena vilevile,” anasema Winga.

Winga anasema kuwa wamekaa wodi siku saba bila kupona, ndugu wameamua kumpeleka kwa waganga wa kienyeji wanadai huenda kafanyiwa mambo ya ushirikina ambayo hospitali hawawezi kuyatibu.

“Mimi nimewazuia nimewaambia wasiende kwa mganga wamekaidi wameenda kwa kutumia nguvu mpaka tumekosana nilikwishaona tena mzazi wa hivi lakini alipona hawajaniamini,” alisema Winga.

Diwani wa Nyankende, Doa Limbu, anasema kuwa huenda mama huyo alikuwa haudhurii kliniki vizuri wakati wa ujauzito kwani tatizo lingebainika wakati mimba ikiwa ndogo au alipokuwa anakaribia kujifungua.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Ushetu, Dk Matindo Athuman anasema kuwa kichaa cha mimba kinatokana na shinikizo la damu au kuwa na vichocheo  vya mwili ambavyo havipo kwa mtu huyo.

Dk Athumani anasema kuwa mbali na hilo pia inatokana na hali aliyonayo mjamzito nyumbani, kama alikuwa akipata mawazo mabaya aliyokuwa akifanyiwa kabla na baada ya ujauzito wake.

“Sisi huwa tunaangalia mazingira aliyotoka alikuwa akiishije, inawezekana purukushani za huzuni zinaweza kusababisha uchungu kwa muda mrefu au hofu,” anasema Dk Athumani.

Dk Athumani anasema kuwa kichaa cha mimba pia wanaangalia matunzo ya awali ya mimba, maisha yake na matokeo ya uzazi kwa kuangalia kisaikolojia kama hali iko sawa.

“Kuna wanaoumwa kidogo, kiasi na zaidi hadi kufikia kudhuru mtoto ama kujidhuru mwenyewe pia mtoto akiwa mchanga kichaa cha mimba kinaweza kwenda hadi miezi sita baada ya kujifungua,” anasema Dk Athumani.

Anasema jamii inawahukumu wenye kichaa cha mimba bila kujua ni tatizo la kisaikolojia linalotakiwa msaada kabla ya madhara makubwa kutokea ya mama kujidhuru au kudhuru mtoto.

Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto, Mkoa wa Shinyanga, Halima Hamis, anasema kuwa vifo vya watoto wachanga kwa mwaka 2021 vilikuwa 665 na vifo vya wajawazito mwaka huo vilikuwa 50.

“Mjamzito anashauriwa ahudhurie kliniki mara nne na baada ya kujifungua ndani ya siku tatu sababu kipindi hicho mama anakuwa kwenye hali ya hatari ya uangalizi kuhusu maendeleo ya afya yake na mtoto,” anasema Halima.

Wataalamu wa afya ya akili wanasema ujauzito hupunguza seli za ubongo katika baadhi ya sehemu za ubongo wa mwanamke ili kumwezesha kuhusiana vyema zaidi na mtoto na kujiandaa kwa majukumu ya umama.

Shirika la Utangazi la BBC nchini Uingereza limebainisha kuwa uchunguzi uliofanywa kwa wanawake 25 nchini humo waliokuwa wameshika mimba kwa mara ya kwanza ulionesha mabadiliko hayo kwenye ubongo hudumu hadi miaka miwili baada ya mwanamke kujifungua.

Wataalamu hao wanasema inadhaniwa kwamba wanawake wanaopata kichaa cha uzazi wanakuwa na viwango vichache vya homoni inayoitwa Estradiol (Estradiol Deficiency).

 

 

 

1 comments

Comments are closed.