Dalili, namna ya kusaidia anayetaka kujiua

DAR ES SALAAM; JUZI na jana baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa na taarifa kuwa, Frateri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga, Rogassion Massawe amejinyonga hadi kufa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Almachius Muchunguzi amenukuliwa akithibitisha kuwa, tukio hilo lilitokea katika Nyumba ya Malezi ya Magamba aliyokuwa akiishi.
Kamanda huyo alinukuliwa akibainisha chanzo cha kujiua frateri huyo kuwa ni uamuzi wa walezi wake kutompitisha kuendelea na hatua inayofuata baada ya ufrateri.
Kwa Kanisa Katoliki, baada ya ufrateri mhusika huingizwa katika hatua ya ushemasi na kisha kupewa Daraja ya Upadri ni hatua ya ushemasi kabla ya kufikia upadri.
Tukio hilo linakuja siku chache baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa Kanisa la Methodist Afrika, Joseph Bundala (55) kukutwa amekufa huku ikidaiwa kuwa amejinyonga.
Ilidaiwa kuwa tukio hilo lenye utata na ambalo bado liko kwenye uchunguzi wa vyombo vya dola kubaini ukweli wake, linadaiwa kufanyika kwa kamba ndani ya ofisi yake iliyopo kanisani hapo katika Mtaa wa Meriwa, jijini Dodoma. Mwili wa Askofu Bundala uligundulika saa 1:00 usiku ukiwa unaning’inia ofisini kwake.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari,  kiongozi huyo wa kiroho ameacha waraka mrefu ukieleza sababu za kuchukua uamuzi huo unaokwenda kinyume cha sheria za nchi na Amri za Mungu kuwa ni madeni na mgogoro ulioko katika uendeshaji wa shule binafsi.
Kumekuwa na matukio kadhaa ya watu kujaribu na wengine kufanikiwa kujiua licha ya kuwa Maandiko Matakatifu yanakataza kuua nafsi ama iwe yako, ya mwanao, nduguyo au yeyote. Kwa mujibu wa sheria za nchi, kuua na kujaribu kuua ni kosa.
Ndio maana kwa mujibu wa uchunguzi, inapobainika bila shaka kuwa mhusika amejiua kweli na hakuuawa, mara nyingi huwa hapati heshima za kuzikwa kiroho au kijeshi kama ni askari. Hata kimila, hufanyika ‘ibada’ kadhaa kukomesha balaa hilo.
     Kwanini watu huamua kujiua
Watu mbalimbali wanasema sababu kubwa na ya jumla ya watu kujiua ni kukata tamaa baada ya kujitambua kuwa hawana mbinu mbadala ya kujiondoa katika mtanziko unaowakumba.
Miongoni mwa mambo mengi, inaelezwa kuwa kujiua kunaweza kuwa kumesababishwa na mtu ni kujikuta mikononi mwa adui hasa kwa askari ingawa pia ni kosa, pamoja na kudhani kuwa kosa alilofanya mtu halisameheki na ni la kipekee.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kulemewa madeni, kuua, kufanya kitendo cha aibu kama kuzini na maharimu au kubaka na kukata tamaa, kufilisika kutokana na ugumu wa maisha au changamoto ya afya ya akili. Wengine wanasema, watu huamua kujiua ili kukwepa aibu au adhabu iliyo mbele yao hata baada ya kufeli masomo au kusingiziwa.
Kimsingi, kati ya sababu zozote zilizotajwa awali na nyingine ambazo hazijabainishwa katika makala haya, hakuna hata moja inayohalalisha kosa hilo.
Kwa mujibu wa kipeperushi cha Idara ya Kinga, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma katika Wizara ya Afya kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kuzuia Kujiua Duniani, Septemba 10, 2023, baadhi ya visababishi vya watu kujiua ni pamoja na msongo mkubwa wa mawazo, hofu, matumizi ya dawa za kulevya, matumizi ya pombe kupita kiasi na unyanyasaji katika jamii ukiwamo wa kijinsia dhidi ya watoto na wanawake.
Mkurugenzi wa shirika la kimataifa la kutetea uhai la Human Life International (HLI), Kanda ya Afrika kwa Nchi zinazongumza Kiingereza, Emil Hagamu, anasema: “Mtu kuamua kujiua ni matokeo ya kukata tamaa kwa kiwango cha juu kiasi cha kujivua na kupoteza thamani ya uhai wake.”
Hagamu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirika la Kutetea Uhai (Prolife) Tanzania kuwa kukata tamaa huko  humfanya mtu husika ajione asiye na mbadala wa anachokifikiria yaani anakosa tumaini lingine na kuona kifo ndicho suluhisho pekee analostahili.
Kwa mujibu wa jarida la Psychology Today, kuna sababu kadhaa za watu kuua au kujiua. Sababu kubwa ya kwanza ni kwamba wale wanaoamua kuua huwa wamefikia ukomo wa kuvumilia na hivyo wameugua ugonjwa wa ‘ukomo’.
Ugonjwa huo unatokana na mgandamizo mkubwa wa shinikizo kwa kuwa mtu hufikia mahali akaona kwamba hapati tena ufumbuzi wa kile alichokusudia na matokeo yake, hujikuta anarudia mle mle ambamo tayari pamemchosha.
Jarida linasema watu hao ni wagonjwa kwani nafsi zao zimevia na zimeshindwa kutoa majibu mapya.
Mwandishi Elias Mhegera aliwahi kumnukuu mwanasaikolojia Felicitas Heyne katika https://mhegera.wordpress.com, akisema watu wanaofikia uamuzi huo huwa wamejengewa au kujijengea ukatili.
 Anaandika: “Inawezekana kujiua au kuua kunatokana na kufanyiwa ukatili kiasi kwamba, mtu anaamua kuchukua ufumbuzi kulingana na akili yake inavyomtuma…”
Kwa mfano wengine huwa walevi wa kupindukia, wengine huwa na aibu tele kutokana na yaliyowasibu na wengine huamua kujitenga na jamii zao.
Wataalamu wa mambo ya kijamii na kisaikolojia wanasema, si kweli kwamba tangu hatua za mwanzo hadi mwisho mtu anayejiua ‘humaliza mwendo’ akiwa na wazo hilo hilo, badala yake wanasema katika hatua za kutapatapa kabla ya kukata roho, hufikia hatua mtu akatamani kupata msaada na kuokolewa.
Uchunguzi wa HabariLEO kupitia vyanzo mbalimbali umebaini kuwa, wanaokengeuka na kuamua kufanya hatua hiyo iliyo kinyume na mapenzi ya jamii, serikali na hata Mungu, hujaribu au hujiua kwa kutumia njia mbalimbali ikiwamo kujiua kwa silaha kama bunduki, kujichoma kisu, kujirusha majini na hata kunywa sumu na kutimiza azma yao ya kuitelekeza familia na jamii.
    Kumtambua mwenye mwelekeo wa kujiua
Vyanzo vinasema wapo pia ambao kabla ya kufa kimwili, tayari walikuwa wamekufa kisaikolojia na kifalsafa kwa maana ya kwamba, mawazo yao yalishawatuma kwamba maisha hayana maana tena kiasi kwamba kuua au kujiua kumekuja kama hitimisho la fikra hizo zinazoweza kuwa zimejengeka kwa muda mrefu.
Chanzo kimoja kinasema: “Wapo ambao hugundua dakika ya mwisho kwamba walifanya makosa makubwa na wala hawawezi kurudi nyuma kwa hiyo hitimisho la mwisho linakuwa ni kuyakatisha maisha yao.”
Moja ya dalili kuu kwa watu wanaotaka kujiua ni kukata tamaa na kujitenga.
 Hagamu anasema: “Mtu anakuwa kila wakati anajitenga, hataki ushirikiano wala mawasiliano na wengine….”
Kumsaidia anayetaka kujiua.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya kisaikolojia, daima kuwa makini dhidi ya matamshi ya kujiua.
“Mtu atakaposema anafikiria kujiua, jua kuwa hiyo ni ishara wazi ya kujiua. Tafuta msaada kutoka kwa mtaalamu haraka iwezekanavyo,” kinasema chanzo kimoja mtandaoni.
Kinaongeza: “Ikiwa mtu atakuambia ya kwamba unastahili kuweka siri nia yake ya kujiua, usikubali. Katika hali yoyote ile hustahili kuweka siri hiyo inayoweza kusababisha kifo cha mtu huyo.”
Wataalamu wa sheria na mambo ya kiimani wanasema bayana kuwa, kumtunzia siri ya kujiua mta anayetaka kujiua ni kusaidia au kushiriki kufanikisha kifo chake.
Inasemwa wazi kuwa, kuweka siri ya mtu anayetaka kujiua kutakuwa mateso kwako na kutakusumbua maishani kama atafanikisha azma hiyo mbaya ya kujiua.
Mhegera anaandika: “Chukua hatua zitakazozuia mtu huyo kujiua….”
Katika chapisho lake, Mhegera anasema: “Usishtuke. Anayetaka kujiua ana mawazo mengi na ikiwa utashtuliwa na kinachosemwa, anayetaka kujiua atakuwa na msongamano wa mawazo zaidi. Tulia.”
Anaongeza: “Sikiliza kwa umakini anachotaka kusema mtu huyo. Mruhusu aongee. Sikiliza kwa karibu ndipo uweze kumsaidia iwezekanavyo na ujue kinachosababisha hisia zake za kujiua. Mfariji mtu huyo na maneno ya faraja. Tumia akili uliyonayo kumshauri. Kuwa mpole na anayejali kwa vyovyote iwezekanavyo.”
Machapisho mbalimbali yanasisitiza kuwa, katika kumsaidia anayetaka kujiua, mfanye atambue ya kwamba unamjali. Mwambie na uoneshe ya kwamba unamjali.
“Usimhukumu kwa matendo yake. Usibatilishe anachosema au kuhisi. Msaidie na umjali, si kumhukumu, lakini tafuta usaidizi haraka iwezekanavyo. Msaada waweza kutoka kwa wahusika wa familia yake au marafiki, mradi wasisababishe kujinyonga kwa jamaa yao, au mfanyakazi wa dharura au mtaalamu anaweza kuwa wa maana kwa kutoa usaidizi,” linasema toleo moja ya gazeti la Amkeni.
Hagamu wa Prolife Tanzania anasema: “Ikiwa mtu huyo yuko katika hatari kubwa ya kujiua, usimuache peke yake, hata kwa sekunde chache. Mtengenezee mazingira ya kutojiona wala kuwa katika hali ya upweke.”
Anaongeza: “Zingatia kwamba, kumshauri mtu huyo kwa maneno tu kwamba usijiue usijiue, hakutoshi maana si rahisi kuacha kwa maneno hayo tu, anaweza kupata upenyo akatekeleza ubaya huo, dawa pekee ni kumfuatilia na kuwa karibu naye kwa upendo.”
Katika mazungumzo Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Ngorongoro, Benezeth Bikizo anasema: “Weka mbali naye zana zote hatarishi anazoweza kutumia kama njia ya kujiua mfano kamba, visu na sumu.”
Kuwa makini kwa kuwa wataalamu wa mambo ya jamii wanasema mara nyingi mtu anayefanya jaribio la kujiua akaokolewa, hujaribu tena kufanya hivyo na anaporudia hutumia mbinu kali zaidi kufanikisha dhamira yake.
Aidha, vyanzo mbalimbali vya kisaikolojia vinasema wanawake wanaongoza kwa kufanya majaribio ya kujiua, lakini hawafanikiwi kama ilivyo kwa wanaume ambao idadi ya majaribio yao ni ndogo, lakini hutumia mbinu na nia ‘nzito’ zaidi kiasi cha kufanikiwa kutenda kosa hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button