Dar ina uhaba wa magari ya wagonjwa

MGANGA Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam, Rashid Mfaume amesema mkoa huo unakabiliwa na uhaba wa magari 24 ya kubebea wagonjwa.

Dk Mfaume amebainisha kuwa mahitaji ya mkoa huo kwa sasa ni jumla ya gari 36 ambapo kwa sasa magari ambayo yapo na yanafanya kazi ni 12.

Ameeleza hayo alipozungumza na HabariLEO kuhusu uhaba huo na jitihada ambazo zinafanyika kumaliza tatizo hilo.

Alisema mahitaji hayo na mengine katika vituo vya afya yanaweza kuongezeka kadri ya muda unavyokwenda kwa kuwa mkoa huo unapokea watu wengi kutoka mikoa mingine.

Alisema awali kulikuwa na uhaba wa magari 25 lakini hivi karibuni Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imenunua gari moja la kubebea wagonjwa na kufanya uhitaji kubaki magari 24.

Alisema idadi ya wagonjwa na wajawazito wanaofika hospitalini ni kubwa na wanaopata changamoto na kuhitaji rufaa ni wengi, hivyo yanahitajika magari ya wagonjwa ya kutosha muda wote kwa ajili ya kuwasaidia kutoka hospitali moja kwenda nyingine.

Alitoa mfano kuwa mwaka jana kulikuwa na zaidi ya wajawazito 100,044 waliofika hospitali na vituo vya afya kwa ajili ya kujifungua na sio wote wanajifungua kawaida, wengine wanapata changamoto ambazo zinahitaji rufaa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button