Dar kuboresha miundombinu kukabiliana na mvua

MKOA wa Dar es Salaam unafanya jitihada za kutengeneza mifumo ya utoleaji wa maji kuelekea baharini ili kukabiliana na hali ya mafuriko inayoweza kutokea katika kipindi hiki cha mvua.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kufungua kongamano la Kimataifa kuhusu utumwa na maisha baada ya utumwa katika historia ya Afrika lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Amesema jitihada hizo zinaendelea kufanyika ikiwa ni njia ya kuchukua tahadhari baada ya kuelezwa kuwa kutakuwepo na mvua kubwa ya El-nino.

Advertisement

“Lakini mnakumbuka mabadiliko ya tabia nchi yameathiri kwa kiasi kikubwa bahari imepanda juu na kwa mantiki hiyo baadhi ya mito badala ya kupeleka maji baharini wakati fulani maji ya bahari yanakuja nchi kavu.

“Kwa hiyo ni athari ya mabadiliko ya tabia nchi, tunatumia mbinu zote kuhakikisha mabadiliko ya tabia nchi hayatuathiri kwa sehemu kubwa na kuendelea kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi,” amesema.

Chalamila amesema siku chache zilizopita alizunguka Mkoa wa Dar es Salaam akitoa elimu kuhusu masuala ya ujio wa mvua za elnino ambazo zilikisiwa kuwa zitaleta athari.

“Na mtakumbuka kuwa Dar es Salaam ni moja ya mkoa ambao tunaweza tukasema upo chini sana kutoka kwenye usawa wa bahari na mvua hizi zimenyesha nyingi na tumepokea malalamiko kutoka kwa wananchi kwa baadhi ya maeneo moja likiwa ni mafuriko kwenye baadhi ya maeneo na kubomoa nyumba za watu.” amesema.

Amesema kwa kuwa walishatoa elimu na tahadhari athari hazitakuwa kubwa kwa kuwa Dar es Salaam kuna mito mingi ikiwemo mto mkubwa wa Msimbazi ambao wamejitahidi kuusafisha ili usiwe na athari kubwa.

Mito mingine ni mto Ng’ombe, Mlalakuwa, Tegeta na tuna mito mingine inayopakana na Mkoa wa Pwani.

“Kwa kiasi kikubwa kama ambavyo mvua hizi zingeweza kunyesha bila tahadhari na elimu yoyote madhara yake yangekuwa ni makubwa sana lakini ninaweza kukiri kuwa leo hata ukipita pale jangwani kwa mvua yote ya jana (juzi) iliyonyesha lakini jangwani hatukufunga barabara.” amesema.

Amesema huo ni uthibitisho kuwa mvua zilizonyesha kweli zilikuja mkoa ukiwa umejiandaa ili kukabiliana nay ale madhara ambayo yanaweza yakapatikana.

2 comments

Comments are closed.