Dar kuendesha sensa ya wafanyabiashara

SEPTEMBA mosi mwaka huu, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itaanza kufanya sensa ya wiki moja kwa ajili ya kuwatambua wafanyabiashara waliopo katika eneo hilo pamoja na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya ndani yatokanayo na tozo mbalimbali.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji hilo, Jamaary Satura amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo kuhusu mikakati anayokusudia kuifanya ikiwa ni ndani ya mwezi mmoja tokea ahamishiwe hapo akitokea Halmashauri ya Shinyanga.

Advertisement

Satura amesema kwa kufanya hivyo wataweza kuwatambua wafanyabiashara wa eneo hilo kwa heshima na fedha zao, kwa kuamini wanatoa fedha ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na serikali isiende mifukoni mwa watu ambao ni ‘makanjanja’.

“Kwa hiyo miongoni mwa majukumu ambayo katika wiki za kwanza nimejaribu kuyafanya kiukamilifu ni kuusoma mfumo wetu wa mapato wa jiji, namna gani ambavyo tunakusanya mapato yetu, maeneo gani ambayo tunadhani yana mianya ya uvujishaji wa mapato na nini ambacho tunaweza kukifanya ili kuweza kudhibiti.

“Kwa haraka kabisa tumebaini kwamba mapato yetu tuliyokusanya tunaweza tukakusanya zaidi kuliko ilivyo sasa.

Kwa nini tunaweza kukusanya zaidi ni kwa sababu hatuna orodha sahihi ya wafanya biashara na watu ambao wanapaswa kutulipa kodi zetu.

“Sasa kwa kutokuwa na orodha sahihi hii inatoa mianya kwa watumishi ambao sio waadilifu kuweka viwango vidogo vya tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara wetu lakini wakati mwingine kujinufaisha wao wenyewe kutokana na kutokuwepo kwa hiyo orodha sahihi,” amesema.

Amesema watu hao wasio waaminifu wamekuwa wakijinufaisha kwa kwenda kuchukua fedha na kutoa risiti ambazo nyingine ni bandia pia kumekuwa na leseni ambazo zinashukiwa zinaweza zikawa ni bandia pamoja na vibali ambavyo vinawezekana ni bandia.

“Kwa hiyo tumeshaanda mikakati mingi kabisa na timu ya wataalam namna tunavyokwenda kudhibiti kabisa kwani

tutafanya kama utaratibu wa sensa, tutatumia vishikwambi tutawatumia walimu. Kwa nini tunasubiri Septemba moja ni kwa sababu ni kipindi ambacho walimu watakuwa wamefunga shule,” amesema.

Amesema kazi hiyo itafanywa kwa wiki moja kwa kutumia vishikwambi kama lilivyofanywa zoezi la sensa, litafanyika katika eneo lote la Jiji la Dar es Salaam.

Amesema kwa kufanya hivyo watakuwa na orodha ya watu wote ambao wamekuwa wakilipa lakini fedha hizo zimekuwa zikienda mikononi mwa makanjaja.

Amesema siku hiyo ikifika itatanguliwa na hamasa kubwa kwa wananchi kuarifiwa Jiji linakwenda kufanya usajili wa kuwatambua kwa heshima.

“Kwa kutokuwa na orodha sahihi inaruhusu hata watu ambao zamani walikuwa watumishi wa jiji bado wanaendelea kurudi kwenye maeneo kwa sababu ya mazoea na wananchi waliwazoea kumbe unakuta mtu alishastaafu au mtu ameshahamishwa anarudi kufanya wizi na ubadhirifu.

“Lakini tutakapokuwa na orodha maana yake sisi tutakuwa tunajua nani na nani hawajatulipa tutakapokwenda kule akituambia alimlipa bwana Juma alipita siku fulani sisi tutamfuatilia huyo bwana Juma tutamkamata na tutamwingiza ndani ya mikono ya kisheria.

“Lakini kwa sababu hatuna orodha inatuwia vigumu kujua ni nani ametulipa, nani hajatulipa , nani ametulipa kwa usahihi nan ani hajatulipa kwa usahihi kwa hiyo hilo ni eneo moja la mapato,” amesema.

Amesema serikali imewapa wajibu wa kukusanya mapato ya ndani kutokana na tozo mbalimbali, kama kiongozi mkuu wa watumishi ni lazima aratibu vizuri suala hilo la mapato kwa sababu wakikusanya vizuri mapato ya ndani itawapa nguvu ya kuwahudumia wananchi vizuri.

Amesema kama wakiruhusu mapato ya ndani yavuje washindwe kukusanya maana yake ni kwamba jukumu lao la kuimarisha utawala halitafanikiwa.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *