MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa ripoti kuhusu takwimu za mawasiliano ya simu nchini inayoonesha hadi Juni mwaka huu laini za simu zilizosajiliwa na zinazotumika nchini ziko zaidi ya milioni 56.22.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na TCRA na kuwekwa kwenye mtandao wao, katika soko la huduma za mawasiliano kampuni sita zinatoa huduma kwa wananchi.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa wingi wa watumiaji wa huduma za mawasiliano ukiwa na laini za simu milioni 9.10 zinazofanya kazi, ukifuatiwa na Mwanza laini milioni 3.37, Arusha laini milioni 3.26, Tabora laini milioni tatu, Mbeya laini milioni 2.96 na Morogoro laini milioni 2.94.
Mikoa mingine ni Dodoma wenye laini milioni 2.86, Kilimanjaro wenye laini milioni 2.21, Tanga laini milioni 2.09, Geita laini milioni 2.05, Mtwara laini milioni 1.64, Shinyanga laini milioni 1.64, Pwani laini milioni 1.63, Kagera milioni 1.56, Mara milioni 1.55, Ruvuma laini milioni 1.51, Manyara milioni 1.44, Iringa milioni 1.43, Singida laini milioni 1.39.
Mkoa wa Kigoma una laini milioni 1.25, Songwe laini milioni 1.13, Lindi laini milioni 1.08, Rukwa laini milioni 1.00, Njombe laini 897,453, Katavi laini 658,809, Unguja 414,763 na Pemba 186,369.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa idadi ya watumiaji wa laini za simu zilizosajiliwa inaongezeka mwezi hadi mwezi na mfano ni taarifa ya mwezi Juni mwaka huu ambayo kwa mitandao mingi ya simu usajili wa laini mpya uliongezeka.
Kuhusu matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, taarifa hiyo inaonesha kuwa kampuni ya Vodacom inaongoza wa watumiaji wa huduma za kifedha za M-pesa kwa kuwa na wateja zaidi ya milioni 14.52 mwezi Juni mwaka huu ikifuatiwa na kampunni ya Tigo yenye wateja milioni 9.74.
Taarifa hiyo ilisema katika huduma za kifedha mtandaoni kwa kipindi cha Juni mwaka huu zaidi ya shilingi bilioni 11.60 zilifanyika ukilinganisha na taarifa za Januari mwaka huu ambapo jumla ya shlingi bilioni 10.35 zilifanywa kwa njia hiyo.
Ripoti hiyo inaonesha kampuni ya Vodacom inaongoza katika mauzo sokoni kwa kuwa na asilimia 31 ya wateja wote wawanaotumia laini za simu, ikifuatiwa na kampuni mbili za Tigo na Airtel ambazo kila mmoja ina asilimia 27 ya hisa, Halotel asilimia 12, TTCL asilimia tatu huku Smile ikiwa na asilimia sifuri.