Dar wakusanya kodi Sh trilioni 10.5 miezi sita

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amesema Mkoa huo umevunja rekodi ya kulipa kodi kwa kipindi cha miezi sita kwa mwaka 2022, ambapo Sh trilioni 10.528 zilikusanywa.

Amewahakikishia wafanyabiashara na wawekezaji kuwa Serikali imedhamiria kuweka mazingira bora ya biashara pamoja na kutatua changamoto za wafanyabiashara.

Makalla amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Biashara mkoani humo, lenye lengo la kusikiliza changamoto za wafanyabiashara na kuweka mikakati endelevu ya  utatuzi wa changamoto za kibiashara zitakazowasilishwa.

Amepongeza jitihada zilizofanywa na wafanyabiashara wa mkoa huo na kwamba hatua hiyo imefanikiwa kutokana na mazingira mazuri yaliyotengenezwa na serikali ya kufanya biashara.

“Hatujasikia watu kukimbizana na wengine hata kufunga biashara, hivyo kiwango kilichokusanywa kinatokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Rais,” amesema Makalla na kuongeza kuwa Dar es Salaam bado ina nafasi kubwa ya kuchangia pato la Taifa.

Amesema kwa mantiki hiyo ndio maana serikali iko karibu na wafanyabiashara kuhakikisha kuna usalama na mazingira bora ya biashara na hata kilipoibuka kikundi cha kihalifu maarufu kama panyaroad kilidhibitiwa.

Amewahakikishia ulinzi na usalama wafanyabiashara ikiwa ni pamoja na kukomesha matukio yote ya uhalifu.

Akizungumza katika mkutano huo, mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA),Tirison Kabuje amesema asilimia 70 ya mapato ya kodi ikusanywayo inatoka Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema kutokana na hilo,TRA imeanzisha  dawati la usajili wa biashara na leseni, ili taarifa zote zikamilike kwa wakati  pamoja na kuanzisha dirisha la usajili la TIN binafsi Kwa njia ya mtandao.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x