MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amewataka wakazi wa jiji hilo wajipange kufanya biashara saa 24.
Pia Chalamila alisema usafiri wa mabasi ya mwendokasi utakuwa wa saa 24 ili kupunguza misongamano wakati wa mchana.
Alisema hayo Dar es Salaam juzi usiku alipozungumza kwenye kipindi cha Ardhio kilichorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
Chalamila alisema kumekuwa na changamoto ya watu wanaotaka kununua bidhaa katika eneo la Kariakoo hivyo kusababisha mabasi ya mwendokasi yajae.
“Hata Rais (Samia Suluhu Hassan) aliuliza kwanini hatujaamua kufanya biashara saa 24 hasa katika mahali kama Kariakoo lakini kwenye mabasi ambayo Rais ametoa fedha nyingi kuwekeza,” alisema.
Aliongeza: “Miundombinu ya mwendokasi ni gharama kubwa kuna karibu Sh bilioni 231.7 na juzi tumesaini mkataba wa mwendokasi kutoka Mwenge mpaka Tegeta, sasa nani atapanda haya mabasi? Ndio maana tukawaza ni vizuri kufanya biashara ya mabasi saa 24…na watu hawa wanaenda wapi, ni vizuri sasa wafanyabiashara Kariakoo wafanye saa 24.”
Chalamila alisema kuna mpango kituo cha mabasi ya Lindi na Mtwara Mbagala Zakiem, kituo cha mabasi ya mikoani na yanayokwenda nje ya nchi cha Mbezi, Ubungo na kile cha Bagamoyo kilichopo Tegeta kuwe na biashara saa 24.
“Oktoba mwaka huu Soko la Kariakoo linakwisha, kabla hatujafungua tutakaa vikao na wadau wa mabenki, wadau wa ulinzi na usalama, wafanyabiashara wenyewe ili tuafikiane kuhusu kufanya biashara saa 24 na tutaanza na eneo hilo la Kariakoo,” alisema.
Kuhusu ulinzi alisema askari wapo kwa ajili hiyo na hakuna kitakachoshindikana kwani pia kuna maeneo yatawekwa taa na kamera za ulinzi pale inapoonekana kuna umuhimu.
“Kama biashara zikifungwa mapema, askari atalazimika kulinda eneo kubwa lakini biashara zikifanyika eneo moja saa 24, maana yake ni kwamba wote watajikusanya eneo moja kubwa na litakuwa kama chambo kwa yeyote atakayetaka kuvunja amani, kwa hiyo kundi dogo la watu litalinda kundi kubwa,” alisema Chalamila.
Aliwataka wafanyabiashara wapunguze malalamiko kwani Rais Samia ameimarisha miundombinu, ameleta wawekezaji, ameondoa tozo na kodi, anawasikiliza wafanyabiashara, hivyo watumie wema na hekima yake kujineemesha.
Kuhusu mgogoro wa wafanyabiashara Kariakoo, Chalamila alisema tume iliyoundwa imeshakabidhi ripoti kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baada ya hapo kitasomwa kilichopendekezwa.
“Dar es Salaam ni Jiji la biashara kwa hiyo, tuna wajibu kuhakikisha yale mambo madogomadogo na makubwa kuhusu wafanyabiashara, tunayashughulikia na huo ndio mwelekeo mkubwa wa Rais Samia,” alisema Chalamila.
Comments are closed.