MIAKA miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan, watanzania 944 na raia wa kigeni 57 wamepata ajira katika mradi wa ujenzi wa daraja la J.P Magufuli, linalounganisha eneo la Kigongo wilayani Misungwi na Busisi wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mwanza Mhandisi Pascal Ambrose amesema ajira hizo zimewanufaisha zaidi Watanzania ambao mbali na kufanya kazi lakini pia wananufaika na ujuzi wa ujenzi wa miradi mikubwa kama wa daraja hilo.
Amesema, wapo Watanzania walioajiriwa katika mradi huo bila kuwa na ujuzi lakini kwa sasa wamejifunza na wanafanya kazi mbalimbali katika mradi wa ujenzi wa daraja hilo.
Aidha, amesema kazi nyingi katika daraja hilo zinafanywa na Watanzania, na hivyo kutoa fursa kwao kushiriki katika ujenzi wa miundombinu lakini pia kuongeza ujuzi katika sekta ya ujenzi.