SERIKALI imesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 18 na Daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140 kumepunguza umbali na mzunguko wa kusafirisha malighafi za sukari kutoka kilometa 140 hadi kufikia kilometa 14 kutoka shambani hadi kiwandani.
Hayo yamesemwa mkoani Kagera na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wakati akikagua ujenzi wa barabara hiyo ambayo inapita katika Kiwanda cha Kagera Sugar kilichopo mkoani humo.
“Kilio kikubwa hapa kilikuwa ni changamoto ya miundombinu kutoka shambani hadi kufika kiwandani, matumaini yangu mara baada ya kukamilika kwa miundombinu hii hata bei ya sukari inaweza kushuka kwani gharama za uzalishaji nazo zitapungua kwa namna moja ama nyingingine”, amesema Kasekenya.
Aidha ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Karagwe kuchangamkia fursa ya kilimo cha Sukari kwani watauza kwa bei nzuri na kukuza pato lao na kupata fursa nyingine za kibiashara.
Katika hatua nyingine, Kasekenya amebainisha kuwa tayari mkandarasi amekwishaanza kazi ya ujenzi wa barabara ya Bugene – Kasulo/Benako (km 60), kwa kiwango cha lami ili kuunganisha mkoa wa Kagera na nchi jirani za Uganda, Burundi na Rwanda.
Kwa upande wake Mhandisi Mshauri Lucas Nyaki, amemueleza Naibu Waziri kuwa mradi wa huo ulikamilika mwezi Septemba, 2022 na kazi zilizobakia ni za kupaka rangi vyuma vya daraja, kuweka alama za barabarani pamoja na kazi za mazingira kama vile upandaji wa miti, upandaji wa nyasi na uchimbaji wa mitaro.
Nyaki ameeleza kuwa sasa mradi huo utakuwa chini ya uangalizi wa mkandarasi huyo kwa muda wa miaka mitatu.
Amesema kuwa mradi umegharimu takribani kiasi cha shilingi Bilioni 31 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 26.548 zimetolewa na Serikali Kuu na Kiwanda cha Kagera wamechangia kiasi cha shilingi bilioni 5.
Naye Mwakilishi wa Kiwanda cha Kagera Sugar Vicent Mtaki, ameishukuru Serikali kwa kukamilisha miundombinu hiyo na sasa gharama zimepungua za usafirishaji lakini pia uwepo wa barabara hiyo unavutia waajiriwa maana wanauhakika wa kufika kiwandani kwa haraka na usalama zaidi.
“Hii barabara na daraja ni mkombozi kwetu kwani takribani miwa 1,600,000 zinakwenda kusafirishwa kwa urahisi katika miundombinu hii uharaka na uhakika”, amesisitiza Mtaki.
Daraja la Kitengule linaunganisha barabara kuu ya Kyaka- Bugene- Benako na barabara ya Kagera Sugar Junction- Kakunyu, katika Wilaya za Misenyi, Karagwe na Ngara mkoani Kagera.