Dart yatumia milioni 3.5/- kukarabati madarasa

Dart yatumia milioni 3.5/- kukarabati madarasa

SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la Dart limefanya ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa na kutoa vifaa vya kujifunza vyenye thamani ya Sh 3,550,000 kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lake na Maendeleo zilizoko wilayani Nyamagana jijini hapa.

Hayo yamesemwa jana na Mfadhili na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Dollocela Ruben wakati wa kukabidhi madarasa hayo kwa uongozi wa elimu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Alisema aliamua kufanya ukarabati wa majengo hayo ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye uboreshaji wa miundombinu ya elimu.

Advertisement

Mbali na ukarabati huo, pia Shirika limekabidhi zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wa shule hizo, ambapo alikabidhi makasha sita za kampasi na kalamu kwa shule zote mbili kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani yao.

Alikabidhi pia mabegi ya shule kwa wanafunzi 42 wanaosoma chekechea, mikeka minne ya kukalia, kalamu, madaftari, makasha mawili ya chaki na sabuni za maji kwa shule zote mbili.

“Kama mzazi nimeona pia ipo haja ya kuchangia katika sekta ya elimu na ndio maana nimeamua kuchangia kidogo nilichokuwa nacho,” alisema na kuongeza kuwa mwaka 2018 alikarabati vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Maendeleo kwa gharama ya Sh 2,500,000.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mussa Lamwe aliushukuru uongozi wa shirika hilo kwa msaada huo na kuwaomba wadau wengine wa elimu kuiga mfano.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Isamilo, Justin James aliushukuru uongozi wa shirika hilo kwa msaada wa ukarabati wa vyumba vya madarasa na vifaa ambavyo vitaongeza hamasa ya wanafunzi kusoma na kuinua kiwango cha taaluma shuleni hapo.

Akitoa shukrani kwa niaba ya walimu wa shule zote mbili, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lake A, Anet Gahanga alilishukuru Shirika hilo kwa ukarabati wa vyumba vya madarasa na vifaa vya wanafunzi.