Darts kutumia smart card
Yatakiwa kuongeza mabasi
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) imeutaka uongozi wa Mabasi ya Mwendokasi (DART) kuanza kutumia tekinolojia ya Smart Card ili kuweza kupunguza kero inayoweza kutokea katika upatikanaji wa tiketi kwa abiria na kudhibiti mapato.
Pia kamati imewataka DART kuweza kuongeza idadi ya mabasi ambayo yataweza kupita kwenye miundombinu ambayo wanaiandaa sasa.
Hayo yamebainishwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya TAMISEMI Justin Nyamoga Wakati wa ziara ya kamati ya kudumu ya Bunge ya TAMISEMI ilipokagua miradi inayotekelezwa na DART katika Mkoa wa Dar Es Salaam.
“Ili kuepuka ulipaji fidia wa mara kwa mara wakati wakuongeza miundombinu tunaihitaji kuhifadhi eneo kubwa la kutosha hasa katika miji inayokuwa ili kuwa na maeneo kwaajili ya uendelezaji wa miundombinu hapo badae,” amesema Nyamoga.
Aidha, Nyamoga amesema sehemu yenye makazi ya watu wengi kuwe na umwagiliaji wa maji wa mara kwa mara ili kupunguza kero na maradhi kwa wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo hasa katika kipindi hiki cha ujenzi.