DAS Mbogwe: Marufuku kuozesha wanafunzi
KATIBU Tawala wa Mbogwe, Dk Jacob Julius ‘Jaju’ amewaonya wazazi wenye tabia ya kuozesha watoto kwa kuwakatiza masomo waache mara moja, kwani kuanzia sasa atakayebainika kukatisha masomo ya mwanafunzi hususani wa kike, ajiandae kwenda jela miaka 30.
Julius ameyasema hayo katika mahafali ya wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya Sekondari ya Masumbwe iliyoko Mbogwe mkoani Geita
Amesema, serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefuta ada kwenye shule za msingi na sekondari za serikali kama hatua ya kuinua kiwango cha elimu hivyo ni wajibu wa wazazi na walezi kuwasimamia Watoto kuhakikisha wanatimiza ndoto zao kielimu.
“Wazazi wanaowakatisha watoto wa kike masomo na kuwaoza kufanya hivyo ni kutenda kosa, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mzazi au mlezi yeyote atakayebainika kumuachisha mtoto shule na kumtaka aolewe.”Amesisitiza Julius.
Aidha, ametumia fursa hiyo kutoa rahi kwa wazazi pamoja na waalimu kuthamini miradi mikubwa ya ujenzi wa shule katika wilaya hiyo inayotekelezwa na serikali.
“Kila mtu awe mlinzi wa mwenzie kuhakikisha miradi mikubwa inalindwa, isihujumiwe, lengo ni kuhakikisha kila mtanzania anapata elimu katika mazingira bora.
“Inasikitisha pale ambapo baadhi ya watanzania wanapata fursa ya kusimamia miradi hiyo kupitia kamati mbalimbali za ujenzi wa shule wanapohujumu miradi kwa kushiriki kukwapua fedha zinazoletwa na serikali,”amesema Julius.
Amesema, uongozi wa wilaya hiyo hautasita kuwachukulia hatua za kisheria na za kinidhamu wale watakaobainika kuhujumu miradi hiyo ambayo ni muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo kama ambavyo tayari baadhi ya watumishi wamechukuliwa hatua kwa matendo ya namna hiyo kwenye moja ya miradi inayoendelea wilayani hapo.