Dawasa kusajili watoa huduma wa majitaka

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza zoezi la usajili wa watoa huduma binafsi na utoaji vibali vya uendeshaji wa magari yanayotoa huduma za usafi wa mazingira Dar esSalaam.
 Usajili huo utafanyika  kwa muda wa wiki mbili kuanzia Juni 18 hadi 22,2023 katika eneo la Vingunguti Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo leo Juni 8,2023 Afisa Biashara DAWASA , Mwajuma Hamza amesema zoezi hilo ni endelevu na linafanyika kila mwaka kwa kushirikiana na watu binafsi ambao ni wamiliki wa magari ya majitaka.
“Huu ni mwaka wa sita tangu tuanze utaratibu huu wa usajili ukiwa na lengo la kupata takwimu sahihi za watoa huduma na kuhakikisha utoaji wa huduma za usafi wa mazingira zinaboreshwa kikamilifu kwenye mkoa wa Dar es Salaam.” Amesema Mwajuma na kuongeza
“Leo  tumeanza usajili na tunatarajia kuendesha zoezi hili ndani ya wiki moja ili kuweza kuwatambua watoa huduma ambao huchukua majitaka kwa wananchi na kwenda kumwaga katika mabwawa yetu yaliyoko sehemu mbalimbali.” Amesema.
Amesema  zoezi la usajili wa magari utahusisha magari ambayo yana usajili wa zamani na magari mapya ambayo yameingia kwenye utoaji huduma hiyo ili waweze kutambuliwa na DAWASA katika uendeshaji wa huduma.
“Kwa magari yaliyosajiliwa awali, tunawaomba kufika kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki ukiambatana na fomu inayoonyesha ujazo wa gari kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) na nakala yake.” amesema
Aidha,  amesema baada ya muda wa usajili kuisha, yeyote atakayekutwa anatoa huduma ya uondoshaji na usafirishaji wa majitaka katika eneo la huduma la DAWASA bila kibali hai cha uendeshaji atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Nae,  Mrisho Mataula ambaye ni mwendeshaji wa magari yanayotoa huduma ya majitaka ameipongeza DAWASA kwa zoezi la usajili ambalo wanaliendesha kwani litawasaidia kwa kiasi kikubwa kutambulika na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.
Amesema wamekuwa wakishirikiana na DAWASA kwenye maeneo ya shughuli zao hivyo kwa zoezi hilo la usajili litaweza kusaidia kuondoa usumbufu ambao umekuwa ukijitokeza mara kwa mara na kuondoa baadhi ya kero ambazo zimekuwa zikitokea kwao.
Nae Alex Masumbuko ambaye ni mjumbe wa majitaka amewaomba DAWASA kuendesha shughuli hiyo pasipokuwa na usumbufu kwao kwani wanapoendesha zoezi hilo na wao wanakuwa  wanaendelea na shughuli yao ambayo wanaifanya katika kutoa huduma.

Habari Zifananazo

Back to top button