Dawasa waboresha mifumo ya maji Kisarawe

Dawasa waboresha mifumo ya maji Kisarawe

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA – KISARAWE), inatekeleza kazi ya maboresho ya mfumo wa kusambaza maji kwa wateja wa taasisi kwa kuboresha miundombinu ya maji iliyorithiwa kutoka kwa Mamlaka ya Majisafi Kisarawe (KUWASA).

Akizungumzia matengenezo hayo yanayoendelea katika eneo la ofisi za Dawasa Kisarawe, Msimamizi wa Mradi, Erasto Mwakilulele alisema matengenezo yameanza na kazi inatarajiwa kukamilika wiki ijayo.

“Lengo la kazi hii ni kuwezesha upatikanaji wa huduma kwa wateja wa taasisi ambao hawana maji baada ya mfumo kushindwa kutoa huduma,” alisema Mwakilulele.

Advertisement

Alisema lengo la matengenezo hayo ni kusaidia kuongeza upatikanaji wa huduma kwenye maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa maji ikiwemo hospitali ya Kisarawe, jeshini, wateja wote wa mnarani zikiwemo ofisi za Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mlimani TV, Radio Free Africa (RFA), TTCL, Wapo FM Radio na Clouds FM Radio.

Wateja wengine ni pamoja na shule ya sekondari Minaki.

Alisema kazi inahusisha utoaji wa toleo la maji kutoka kwenye bomba kubwa la inchi 16 na kupeleka kwenye tangi la lita 135,000 lililopo Kisarawe na kazi ya kupeleka maji kwa wateja kwa kutumia bomba la inchi nne.

Alisema kazi inatekelezwa kwa kutumia mapato ya ndani ya Mkoa wa kihuduma Kisarawe.

“Tumeona kuna kila sababu ya wateja wetu kupata huduma na hivyo tumeamua kufanya maboresho haya ili huduma iweze kupatikana muda wote,” alieleza Erasto.

Wakati huo huo Dawasa imesema inaendelea kufanya maboresho makubwa ya miundombinu ya majisafi eneo la Tabata Kisiwani ili kuhakikisha huduma ya maji inamfikia kila Mwananchi.

Imesema eneo la Tabata Kisiwani limekuwa na changamoto ya  kuvuja kwa maji mara kwa mara kutokana na ubovu wa miundombinu lakini kupitia maboresho hayo imefanikiwa kupata ufumbuzi wa kudumu.

Meneja wa Dawasa Tabata, Boniphace Ole, alisema kazi ya maboresho imeshaanza na inatekelezwa usiku na mchana na kukamilika kwake kutamaliza changamoto ya upotevu wa maji eneo la Tabata Kisiwani.