DAWASA yaanza kusafisha visima Dar

MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA), imeanza kuvitambua na kusafisha visima vya maji vilivyopo jijini Dar es Salaam, ili kukabiliana na uhaba wa maji katika Mkoa huo.

Dawasa wakiongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Cyprian Luhemeja, wameanza kazi ya kusafisha visima vya Ilala Bungoni na Olympio Upanga.

Akizungumza na HabariLeo, Luhemeja, amesema kazi ya kusafisha visima hivyo inaendelea lengo ni kuwezesha kisima hivyo kutoa huduma katika kipindi hiki cha ukame.

Advertisement

Amesema Kisima cha Bungoni kina uwezo wa kutoa lita 6000 za maji kwa saa, wakati Kisima cha Olympio, kimeshasafishwa na sasa kitaingizwa kwenye mfumo rasmi wa maji na kwamba kina uwezo wa kuzalisha lita 336,000 kwa siku.

Kusafishwa visima hivyo ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alilolitoa juzi na kuwataka Dawasa kufufua visima 197 ambavyo vilifanyiwa upembuzi yakinifu na wataalamu mwaka 1997.

Tayari mitambo hiyo imetolewa jana na kusambazwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam kwa sasa inakabiliwa na upungufu wa maji wa lita milioni 240, ambapo mahitaji rasmi ya maji kwa Jiji la Dar es Salama ni lita milioni 540 kwa siku, na hivi sasa inapokea maji  lita milioni 300 kwa siku.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *