DC aagiza madalali wakamatwe

DAR ES SALAAM :MKUU wa Wilaya Temeke, Sixtus Mapunda, ameagiza kutafutwa na kukamatwa, kisha kufikishwa mahakamani wote wanaouza viwanja vya NSSF eneo la Toangoma, wakati wakifahamu kuwa maeneo hayo si yao.

Serikali imewataka wote waliovamia eneo la NSSF lililopo Toangoma, Mtaa wa Malela Wilaya ya Temeke kuondoka na haitaruhusu mtu kupora haki ya mwengine.

Advertisement

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda alipokuwa na wananchi waliovamia eneo la NSSF na kueleza kuwa kuanzia Jumanne Juni 18, 2024, ubomoaji wa majengo yote ya wavamizi utafanyika kwa kuanza na yaliyojengwa katika maeneo ambayo yamepangwa kwa ajili ya huduma za kijamii, ikiwemo barabara, miundombinu ya maji, shule, kituo cha afya na kituo cha polisi.

Kwa upande wake Meneja Miliki wa NSSF, Geofrey Timoth amesema wale walikuwepo mwaka 2022 ambao waliingizwa katika mpango wa matumizi ya ardhi wa eneo hilo wataelekezwa mambo ya kufanya, ili waweze kuishi kwa amani na kusisitiza kwamba NSSF tayari imeweka mpango wa matumizi na kuendelea kuwaacha wanaovamia maeneo hayo ni kufifisha juhudi za uwekezaji.

Katika hatua nyengine Sixtus Mapunda ameagiza kutafutwa na kukamatwa ili wafikishwe katika vyombo vya sheria wale wote wanaouza viwanja vya NSSF katika eneo hilo la Toangoma huku wakifahamu fika kuwa maeneo hayo si maeneo yao.