DC aonya sungusungu kujigeuza wanasheria, mahakimu

MKUU wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Jamuhuri William amekemea tabia ya askari wa jeshi la sungu sungu kujigeuza wanasheria na mahakimu baada ya kukamata watuhumiwa akisema vitendo hivyo vinaminya haki za wananchi.

Jamuhuri ameeleza hayo leo katika mahojiano maalumu na HabariLeo ikiwa ni siku chache baada ya kuzindua wiki ya sheria ndani ya halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale.

Amesema wilaya yake inatambua kazi nzuri ya kulinda amani inayofanywa na sungu sungu lakini hawapaswi kujivisha mamlaka ya kisheria ingali hawana mamlaka ya kusikiliza kesi na kutoa hukumu kwa watuhumiwa.

Ameeleza inashangaza kuona watuhumiwa wa kesi za wizi na matukio ya ukatili wa kijinsia wanapokamatwa ndani ya vitongoji na vijiji askari na viongozi wa sungu sungu wao ndio huamua kusikiliza kesi na kutoa hukumu.

“Wanachukua hatua ambazo ni kinyume cha sheria, wana faini zao ambazo ni kubwa sana, kuna kesi ambayo kuna kijana kwenye kijiji cha Bukulu, kata ya Katita, aliiba kuku lakini faini aliyotozwa ni shilingi laki nne.

“Kuna mwingine kwenye kata ya Nyang’hwale alituhumiwa kutembea na mke wa mtu, akatozwa shilingi milioni moja, na hiyo milioni moja wakagawana wao viongozi wa sungusungu pamoja na viongozi wa kijiji.”

Amesema suala hilo linazikumbusha mamlaka za kisheria kuwa ipo haja ya kuwafikia kwa ukaribu wananchi na viongozi wa kijamii kuondoa makando kando yanayominya haki za wananchi na pengine kuchagiza tatizo la rushwa.

Jamuhuri amewataka makamanda wa sungu sungu wilayani humo kuendelea kutoa ushirikiano wa kulinda amani na usalama pasipo kujichukulia sheria mkononi na kutoa hukumu kwa watuhumiwa.

Habari Zifananazo

Back to top button