DC apongeza mgodi kuwajali wafanyakazi

MKUU wa Wilaya ya Tarime, Michael Mntenjele ameeleza kufurahishwa na namna mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara unavyojali familia za wafanyakazi wake kiasi cha kuwaalika kwenda kuona wanavyofanya kazi.

“Tumeendelea kuwa na ushirikiano mzuri na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara. Kwa niaba ya serikali niwaahidi, tutaendelea kushirikiana nanyi katika kuhakikisha mnafikia dhamira yenu katika viwango vya juu zaidi,” alisema.

Alisema matumaini yake ni kwamba Barrick North Mara itafikia malengo yake kwa kuendelea kuyapa kipaumbele maadili ya msingi ya kuwa na usalama mahala pa kazi wakati wote.

“Uwajibikaji na uadilifu, matokeo chanya, ubia, kuwa na watu wa kiwango cha kimataifa,ukweli, uwazi na uadilifu yatafanya mfikie dhamira yenu,” alisema.

Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati mgodi huo ulipokutanisha wafanyakazi na familia zao na wakazi wa vijiji vinavyozunguka mgodi kwenye siku ya familia.

Siku hiyo yenye kauli mbiu ya ‘kazi na familia’ yalipambwa na maonesho ya shughuli zinazofanyika katika mgodi huo, michezo mbalimbali ya watu wazima na watoto,chakula cha pamoja, vinywaji , muziki na kubadilishana mawazo.

Mgodi wa North Mara upo eneo la Nyamongo wilayani Tarime, mkoa wa Mara ukiendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na serikali kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Meneja wa Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko alisema siku hiyo imewezesha wanafamilia za wafanyakazi kuona kazi zinazofanywa na mgodi sambamba na kudumisha mshikamano na jamii inayozunguka mgodi huo.

Habari Zifananazo

Back to top button