MKUU wa wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, Hassan Ngoma ametoa wito kwa walimu kupunguza idadi ya mikopo wanayokopa katika taasisi za fedha hasa zile zenye riba ‘umiza’ ili kujinusuru na umasikini.
DC ametoa wito huo baada ya walimu kuibua malalamiko kwamba wanaishi maisha magumu kwa sababu wanalipwa mshahara mdogo huku lawama zikielekezwa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kwa kudaiwa kuchangia ugumu huo.
DC Ngoma akieleza namna ‘mikopo umiza’ inavyoathiri walimu kiuchumi
Akizungumza wakati wa ufunguzi Mkutano Mkuu wa Nusu Muhula wa Chama cha Walimu Wilaya ya Ruangwa (CWT), DC Ngoma ameelezwa kusikitishwa na mienendo ya baadhi ya walimu wanaosalimisha hadi kadi zao za benki kwenye taasisi za fedha ili kukopa fedha zinazowalipisha riba za asilimia 60 hadi 70 kwa mwezi.
“Unakuta mwalimu mmoja ana deni benki, Vicoba na michezo zaidi ya miwili ambayo inamlazimu kulipa hadi Shilingi elfu kumi kwa siku, achilia mbali yale madeni ya anayolipa kila mwisho wa mwezi. Katika hali hiyo ni mwalimu gani atapata utulivu wa nafsi?,” mteule huyo wa Rais alihoji.
Alisema inafikirisha mno kuona mwalimu ana madeni mengi na makubwa kiasi hicho lakini bado serikali na jamii inamtegemea afundishe vizuri na kwa weledi ili kumpa matokeo chanya wanafunzi.
Hata hiyo, DC Ngoma amewataka walimu kukubali kubadili mifumo ya maisha yao kwa kuanza kulipa madeni yao yote na kuanza upya ili kupitia mishahara wanayolipwa waweze kuwekeza katika biashara na hatimaye kuinua hali za maisha yao.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya alisema Serikali inawategemea katika kuelimisha taifa na kwamba wakiendelea kukopa mikopo isiyo na tija, hawataweza kufundisha kwa weledi kwa sababu ya kuhelemewa na madeni.
Awali, akizungumza katika mkutano huo, Katibu wa CWT wilayani Ruangwa, Godlisten Kabarata, aliwashauri walimu kuwa wasikivu wakati wote ili wakitoka mkutanoni wawe na mambo ya kujivunia ambayo wakiyafanyia kazi wabadilishe mifumo ya maisha yao.
Kabla ya DC kuhutubia, Mwenyekiti wa CWT Ruangwa, Rafaely Soko ameainisha changamoto kadhaa zinazowakabili walimu kiasi cha kuwanyima nafasi ya kuonyesha uwezo wao katika kutimiza majkumu yao.
Alitaja moja kati ya changamoto hizo kuwa ni malimbikizo madeni yanayotokana na uhamisho wa vituo vyao vya kazi.
Mkutano huo umehudhuriwa na walimu wa shule ya msingi, sekondari, vituo vya elimu, ofisi za wakaguzi elimu na vyuo vya ufundi vya wilaya ya Ruangwa.