DC ataka uadilifu ujenzi Veta Mbogwe
MBOGWE: SERIKALI imepanga kutumia Sh bilioni 2.4 kujenga Chuo cha Ufundi (VETA) wilayani Mbogwe mkoani Geita, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mkakati wa kuwa na vyuo vya ufundi kila wilaya nchini.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Sakina Mohamed, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho.
Akizingumza na viongozi na wananchi wa Kata na Tarafa ya Mbogwe, DC huyo amewataka kusimamia kikamilifu maendeleo ya mradi huo na kuhakikisha hakuna wizi wowote wa mali unaotokea au kufanywa na wananchi.
Amewataka wasimamizi wakuu wa mradi huo kwa niaba ya Veta ambao ni ofisi ya mdhibiti ubora wa elimu Mbogwe, kusimamia kwa uadilifu mradi huo ambao utakuwa wa muhimu sana kwa maendeleo ya Wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine, Sakina ametembelea maeneo ya mgodi katika Kata ya Nyakafulu, ambapo pamoja na mambo mengine, amezungumza na wananchi na wachimbaji wa migodi ya Isanjabudugu na Mahina na kuwataka kuendelea kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria na taratibu za madini, lakini pia kuepuka kuajiri watoto wanaopaswa kwenda shule.
DC huyo pamoja Kamati ya Usalama ya Wilaya, wameanza ziara ya kutembelea kata zote za wilaya hiyo pamoja na vijiji kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi ambapo pia ameambatana na wakuu wa taasisi za serikali wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya huyo pia ametumia fursa hiyo kutoa tahadhari juu ya uwezekano wa kuwepo kwa mvua za juu ya wastani zinazoweza kuleta madhara kwa wananchi hivyo kuwataka wanaoishi maeneo ya mabondeni kuchua tahadhari.