DC ataka wafugaji mjini kufungia mifugo

MKUU wa Wilaya ya Singida, Paskas Muragili amepiga marufuku mifugo yote kuzurura ovyo mjini, badala yake wanaohusika wafuge kisasa kwa kuifungia ndani au waipeleke nje ya mji.

Alitoa agizo hilo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa manispaa hiyo baada ya kuchoshwa na tabia ya baadhi ya wakazi wa mji huo kuwa na tabia ya kuachia mifugo yao kujitafutia malisho katika eneo la mji, hali aliyoieleza kuwa ni kero kwa wanaopanda miti na hata waendesha vyombo vya moto.

Kutokana na kero hiyo, amemwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Jeshi Lupembe kuhakikisha kitengo cha sheria katika halmashauri hiyo kinatimiza wajibu wake kikamilifu kwa kuwachukulia hatua stahiki wote watakaokaidi agizo hilo.

Advertisement

“Kuanzia leo (jana), sitaki kuona mifugo wala makundi ya ng’ombe yakizurura mjini,” aliagiza Mkuu huyo wa wilaya.

Aidha, ameitaka manispaa hiyo kutafuta eneo lingine nje kidogo ya mji kwa ajili ya ujenzi wa machinjio mpya na ya kisasa, badala ya kuendelea kutumia machinjio yaliyopo katikati ya mji ambayo kiuhalisia hayakidhi viwango na hadhi ya mji unaokua kwa kasi wa Singida.

Awali, wakijadili suala hilo, madiwani walitupia lawama kitengo cha sheria wakidai kuwa hakifanyi kazi yake ipasavyo.

Walisema kuwa japo sheria ya kuadabisha wanaoachia mifugo yao kuzurura ovyo mjini ipo, lakini kitengo hicho kimekuwa hakichukui hatua yoyote kali dhidi ya wakorofi hao.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Lupembe alisema ingawa kitengo hicho kipo, kwa sasa hakina watumishi wa kutosha lakini akaahidi wakati juhudi zikiendelea za kuomba watumishi wa kitengo hicho kutoka mamlaka inayohusika, atahakikisha mifugo yote haizururi hovyo tena katika eneo la mji.