DC atimua watumia dawa za kulevya soko la Mabibo

MKUU wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba amewataka wanaotumia dawa za kulevya katika Soko la Mabibo Dar es Salaam kuondoka mara moja.

Aliyasema hayo wakati wa kikao tendaji na wenyeviti wa masoko wa Halmashauri ya Ubungo kilichofanyika juzi ofisini kwake kwa lengo la kutatua kero mbalimbali zilizopo katika masoko ya halmashauri hiyo.

Awali, Mwenyekiti wa soko hilo, Enock Kimwayeya alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa pamoja na miundombinu kutokuwa ya kuridhisha ya soko hilo kwa kuwa bado halijakarabatiwa na kutokana na suala la kutokamilika kwa hati, ipo changamoto inayolikabili soko hilo ni uwepo wa wabwiya unga.

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya hapa kuna shida ya kurejea kwa kasi mateja jambo ambalo halinifurahishi, ukiwa kama mkuu wa ulinzi na usalama, ikikupendeza uwaondoe mateja hao,” alisema Kimwayeya.

Akijibu ombi hilo la Mwenyekiti wa soko, Komba alimhakikishia kuwa mateja hao wataondolewa muda wowote kuanzia sasa na kuwataka wafanyabiashara wa Mabibo kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

“Hili nimelichukua nalifanyia kazi, hatuwezi kuvumilia wabwiya dawa za kulevya kuwepo sokoni, kwanza ni hatari kwa afya zao lakini haileti taswira nzuri kwa soko kujaa mateja,” alisema.

Aidha, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka viongozi wa masoko ya Mburahati na Manzese kuhakikisha wafanyabiashara wanapangwa vizuri na siyo kufunga barabara za sokoni.

Habari Zifananazo

Back to top button