DC atoa neno elimu nje ya mfumo rasmi

MKUU wa Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma, Remidius Emmanuel ameitaka jamii kuelekeza nguvu na kipaumbele katika elimu nje ya mfumo rasmi kama  inavyoelekezwa katika mfumo rasmi.

Amezitaka Kamati za maendeleo ya Kata (WDC) na  serikali za vijiji  kutazama mfumo huo kwa kina na kufanya tathmini kupitia maeneo yao.

Alisema hayo juzi wakati  wa  maadhimisho ya Juma  la Elimu ya Watu wazima yaliyofanyika katika viwanja vya kata ya  Hogoro.

“Katika vijiji vyetu na kata zetu, tunayo makundi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, uwajibikaji kwa sisi tuliopewa dhamana ya utumishi, uongozi pamoja na jamii lazima tuone na kusimamia eneo hili kama kipaumbele,” alisema.

Alisema kuna watu wanaingia mikataba kufanya uamuzi usio sahihi  na kudhulumiwa mali zao na hata  kukosa haki kwa sababu ya kukosa elimu.

“Mafanikio ya kuelimisha jamii kunapunguza migogoro inayotokana na watu kukosa uelewa, ingawa tunalo jukumu la kukabiliana na sababu zinazosababisha watu kukosa elimu katika mfumo rasmi,” alisema

Alisema kuwa serikali imeweka mazingira yanayowezesha makundi yote kupata elimu katika mifumo yote.

“Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan pia ametoa fursa ya kurudi shuleni kwa wale waliokatiza masomo kutokana na changamoto mbalimbali kupitia mpango wa Sequip (mradi wa kuboresha ubora wa elimu ya sekondari) na kuitaka jamii kuendelea kuitumia vema fursa hii,” alisema.

Katika hatua nyingine, mkuu wa wilaya alishukuru shirika la DVV International kwa utayari wa kutekeleza mradi wa elimu ya watu wazima wilayani Kongwa kuanzisha kituo maalumu katika kutekeleza program ya ujifunzaji .

Mapema akisoma risala kwa Mkuu wa Wilaya,  Ofisa Elimu ya Watu Wazima  Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa,  Jane Lutego alisema bado elimu ya watu wazima hasa katika kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu hakujapewa kipaumbele  katika usimamizi ukianzia ngazi za jamii.

Maadhimisho hayo yalipambwa na kauli mbiu ‘Kuboresha Mazingira ya Kujifunzia Kusoma, Kuandika na Kuhesabu yanayozingatia Ubora, Usawa na Ujumuishi wa Makundi yote’

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button