MKUU wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuza Ndwata, amepongeza wadau waliohusika na ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa mpira wa kikapu jijini Dar es Salaam.
Uwanja huo uitwao Spider Court, uliopo Oysterbay, Ilala umejengwa na timu za mpira wa kikapu za Spiders na Odigards zote za Dar es Salaam, wakishirikiana na Kampuni ya MMY kupitia kinywaji cha Hennessy, pamoja na chama kinachosimamia Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA).
Akizungumza katika uzinduzi wa uwanja huo mwishoni mwa wiki, Ng’wilabuza Ndwata ameipongeza MMY, pamoja na NBA kwa jitihada zao za kuukuza mpira wa kikapu nchini.
Amesema mpira ni ajira na kwa juhudi, ambazo wamezionesha MMY na NBA, anaamini zitachochea hamasa ya kuupandisha juu mchezo huo.
“Nipongeze kwa wahisani ambao wametujengea uwanja huu, Tanzania ni moja ya nchi za Afrika Mashariki, ambazo zinapambana mchezo wa kikapu uwe miongoni mwa michezo tegemezi kitaifa.
“Naamini uwepo wa uwanja huu utasaidia kuongeza hamasa kwa vijana wadogo na wakubwa na hatimaye kuwa na timu bora ya Taifa ya mpira wa kikapu,” alisema Mkuu wa Wilaya huyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya Spider, ambayo ndio iliyosimamia maboresho kwenye uwanja huo, Lwanga Nikupala, ameeleza kuwa uwanja huo ni miongoni mwa viwanja vinne bora Afrika, ambavyo vimesimamiwa na NBA.
“Uwanja huu una viwango vya kimataifa na vipo vinne Afrika nzima, huu ni upendeleo wa namna yake kwa Tanzania kuwa miongoni mwao, kitu cha msingi tunatakiwa kuutunza na kucheza kwa wingi mpira wa kikapu, ili kupitia mchezo huu tuwe na timu bora,” amesema Nikupala.