MKUU wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Hasan Masala amekemea wananchi wanaovamia na kujenga eneo la hifadhi ya Serikali ilipojengwa rada katika Kata ya Kiseke wilayani humo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara ulifanyika viwanja vya shule ya sekondari Angeline Mabula, wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuhamasisha maendeleo, Masala amesema kuwa serikali itasimamia sheria kwa wavamizi wa maeneo ya umma na haitavumilia viongozi wasio waadilifu wanaouza maeneo hayo na kusababisha migogoro ya ardhi isiyo ya lazima kwa wananchi.
”Kuna viongozi wa mitaa wanashiriki kuuza maeneo ya umma, hawa hatutawaacha, sheria itafuata mkondo wake, lakini wapo pia wananchi wenzetu wanaojenga pale mlima wa rada wakati tulishakataza ndani ya zile mita 60,” alisema.
Pia Mkuu huyo wa wilaya alitumia jukwaa hilo kumshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika Wilaya hiyo, huku akiwahakikishia wananchi utatuzi wa kero sugu ya maji ambayo imekua kikwazo na kwamba serikali imeshatoa fedha kiasi cha Sh milioni 500 kwa ajili ya usambazaji wa maji kutoka tanki kubwa la Buswelu.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, ambae pia ni mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dk Charles Marwa amewataka wazazi kuitumia vizuri wiki ya chanjo kwa kuwapeleka watoto kwenda kupatiwa chanjo katika vituo vya afya, huku akitoa wito pia kwa jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa marburg na kipindupindu kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha.